November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya Bil.11 zaongezwa ujenzi miundombinu Kilosa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Zaidi ya shilingi Bilioni 11 zimeongezwa na Serikali kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 kutoka Bilioni 1.097 hadi kufikia Bilioni 12 kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Fedha hizo ni sehemu ya kuhudumia mtandao wa barabara zenye urefu wa Km 913.67 zinazosimamiwa na Wakala ya Barabara ya Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani Kilosa.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa Mhandisi Harold Sawaki wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa daraja la Ruhembe lenye urefu wa mita 40 itakayogharimu Shilingi Bilioni 1.28 pamoja na kufungua barabara yenye urefu wa Km 2 inayoingia darajani hapo kuunganisha Kata ya Ruhembe na barabara kuu ya Mikumi – Ifakara itakayogharimu Shilingi Milioni 203.

Miradi hii ikikamilika itaenda kuondoa kero ambazo walikuwa wakizipata hapo awali ikiwemo kuwafikisha kwenye barabara pamoja na mahitaji ya kijamii.

“Daraja hili ni kubwa na litaenda kuondoa kabisa kero za wananchi wa kata ya Ruhembe na kuongeza Wakazi hao hawakuwa na njia ya kuwafikisha barabara kuu na hivyo kukosa mahitaji muhimu ya kijamii.

“Wananchi hao ambao ni wakulima wa miwa walikuwa wanapata shida ya kuuza miwa yao na hivyo kupata hasara kubwa “.

Aidha, amesema kwa upande wa ujenzi wa daraja la Berega lenye urefu wa mita 140 linalogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 7.9 kwamba mradi huo unaendelea vizuri na upo katika hatua za mwisho za umaliziaji .

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweza kuongeza bajeti ya fedha na hivyo tunaenda kukamilisha mradi wa daraja kubwa la Berega.

Mhandisi Sawaki ameongeza kusema kuwa kufunguliwa kwa barabara yenye Km 42 ambayo inaunganisha Kata ya Ulaya na Kisanga ambapo kuna kituo cha bomba kuu la kusukuma mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia na hivyo kuwa msaada mkubwa na kuwezesha kuungana na barabara kuu inayoanzia Dumila, Kilosa hadi Mikumi.

“Hii tunaona dhamira kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita namna ilivyodhamiria kuondoa kero za wananchi kwa kufungua barabara mbalimbali ambazo zilikuwa zimefungika na kukata mawasiliano katika pande mbili”.

Hata hivyo amesema TARURA wana mpango mkakati watakayoendelea nayo ya kutekeleza miradi mikubwa na midogo kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo kuna barabara ya kwenda Kisanga kupitia mbuga ya Mikumi yenye urefu wa Km 30 Serikali imetenga fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 ambapo watajenga boksi Kalvati kubwa na kwenda kuondoa tatizo la kuzidiwa na maji na kupelekea kukata mawasiliano.

Kwa upande wa jimbo la Kilosa Mhandisi Sawaki amesema upo mradi mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa barabara ya Ilonga kwenda Mfuluni yenye urefu wa Km 8.9 ambayo imetengewa kiasi cha shilingi Milioni 950 na ni barabara ambayo haijawahi kufanyiwa matengenezo makubwa kwa takribani zaidi ya miaka 30 iliyopita.

“Serikali imeenda kuona tatizo hilo na kuwafikia wanachi wale na kufungua maeneo mbalimbali yenye changamoto ya kufikika. Barabara ile ipo sehemu ya mlimani sana, hivyo mlima ule unaenda kushushwa na kukatwa ili kuwa na mwinuko ambao unaweza kuruhusu vyombo vya usafiri kupita pia kuna kipande kitawekewa zege kwa ajili ya kupaboresha.

Kwa mwaka wa fedha 2023/24 amesema wametengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 4.097 ambazo zitaenda kuhudumia maeneo mbalimbali ambayo yana changamoto ya kufikika ili kuendelea kutoa huduma zaidi na kuondoa kero walizo nazo za barabara, kalvati pamoja na madaraja.

Naye, Mtendaji wa Kijiji cha Ruhembe Bw. Coready Luwanda amesema wananchi wa kijiji hicho walikuwa wakitumia muda mrefu kuzunguka zaidi ya Km 20 ili kwenda kupata huduma za kijamii Mikumi na wakati mwingine walikuwa wakipanga magogo kwenye mto huo ambapo iliwasababishia vifo hususani kipindi cha masika.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo ambapo urefu wa kufika barabara ya lami itakua Km 1.2 na hivyo kuwarahisishia usafiri na kuwaletea maendeleo katika kijiji chao na wananchi mmoja mmoja na hata gharama za bidhaa zitaenda kupungua na pia magari kufika hadi kijijini.