Na Penina Malundo, timesmajira
MKURUGENZI Ukuzaji Tija kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu, Yohana Madadi amesema vijana ni moja ya kundi kubwa katika nchi za Afrika ambao wananafasi ya kuhakikisha masuala ya haki za binadamu ,amani na usalama zinapatikana katika nchi zao.
Kundi la vijana limetajwa kuwa ni kundi ambalo linamchango katika masuala ya ulinzi na usalama katika nchi wanazoishi na kushiriki katika mipango mbalimbali ya ujenzi wa mataifa yao.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Mkutano wa Vijana kutoka nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu na Mkurugenzi Ukuzaji huyo,akimwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema
kutokana na vijana kuwa ni kundi kubwa katika nchi mbalimbali wanamchango wa kuhakikisha amani na usalama katika nchi zao zinapatikana.
Amesema ni vema vijana kuwa wajenzi wakubwa wa amani licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazopitia kutokana na utandawazi ikiwemo masuala ya ajira ambapo yanawafanya kuwa katika mazingira hatarishi.
”Vijana ni muhimu sana katika ujenzi wa nchi zetu ambapo kwa Tanzania katika Sensa ya mwaka 2022, vijana wapo takribani Milioni 21 kati ya Milioni 61 ya watanzania , lakini kundi hili la vijana ndio nguvu kazi kubwa katika mataifa yetu,”amesema na kuongeza
”Hivyo suala la amani na utulivu katika nchi linapaswa kuanzwa na kundi hili,mfano kwa Tanzania makosa mengi ambayo yametokea,Kwa mujibu wa taarifa na Takwimu za Jeshi la Polisi 2019 hadi 2022 zinaonyesha kwamba makosa mengi ni yamefanywa na vijana ambapo zaidi ya asilimia 70 hadi 80 uhalifu mwingi unafanywa na vijana,”amesema.
Madadi amesema suala la usalama na amani ni muhimu linapojadiliwa katika mkutano huo kupitia Mtandao wa Vijana wa nchi za maziwa makuu kuhusu amani na utulivu.”Natoa wito kwa washiriki wanaotoka nchi ya Uganda,Tanzania ,Demokrasia ya Congo,Rwanda na Burundi kuweza kushirikiana katika majadiliano kuhusu vijana ambalo ni jambo muhimu katika maendeleo ya nchi,”amesema.
Kwa Upande wake Afisa Maendeleo ya Vijana Jiji la Dar es Salaam, Happiness Joachim amesema vijana wamehusishwa katika mkutano huo,ikiwa ni kundi ambalo linatumiwa sana katika kupoteza amani ,kupigana vita na vurugu nyingi za kisiasa.
”Naamini kwamba vijana kuhusishwa vijana kwenye midahalo kama hii inayohusu amani na utulivu kutoka nchi mbalimbali hasa za maziwa makuu itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa au kupunguza vita ambazo vinatokea katika nchi jirani ikiwemo DRC,Burundi na Rwanda,”amesema na kuongeza
”Vijana wanapaswa kuendelea kuhusishwa katika mazungumzo haya ya amani kwasababu vijana ndio kundi ambalo lipo katika nchi yoyote hivyo wakihusishwa katika midahalo hii wataweza kulinda nchi zao na kusaidia kuwa na utulivu wa amani bila kusubiria watu wazima ambao wamekuwa wakichochea maugomvi,”amesema
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya taasisi ya Sauti ya Wanawake Ukerewe (SAWAU),Sophia Donald amewataka vijana kuendelea kutunza amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu na kuwasisitiza kutokubali kutumika katika kuharibu amani.
“Nchi yetu inaelekea katika chaguzi mbili muhimu uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani pamoja ja uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,kipindi hicho tunaelewa vija a huwa wanatumika sana kuharibu amani,tunawaasa vijana kutojihusisha na masuala yakuvunja amani.
“Mradi wetu huu ni mradi wakujenga amani kwa vijana ili wananchi wapate maendeleo,tunaangalia ni namna gani tunaweza kuwaelimisha vijana katika masuala ya amani kwakuwa wao wanakuwaga kichocheo chakuvunja amani za nchi zao,”amesema.
Amesema mradi huo ambao unatarajiwa kumalizika Desemba mwaka huu umehusisha vijana kutoka nchi za Tanzania,Congo,Burundi,Uganda na Rwanda.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu