November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSSF yaendelea kugawa miche ya miti kwa wastaafu watarajiwa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendelea na kampeni yake ya kuwapatia miche ya miti wastaafu watarajiwa wa Mfuko huo katika semina zinazoendelea kwenye mikoa mbalimbali nchini za maandalizi ya kustaafu utumishi wa umma kwa wastaafu watarajiwa wa Mfuko huo.

Septemba 19, 2023 ilikuwa ni zamu ya wastaafu watarajiwa wa mkoa wa Mbeya waliopatiwa miche hiyo sanjari na elimu ya maandalizi ya kustaafu utumishi wa umma kwenye ukumbi wa Mkapa jijini humo. Mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa Mhe. Juma Homera.

Viongozi wa PSSSF wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji, Bw. Fortunatus Magambo na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi Bw. Ernest Khisombi kwa niaba ya Mkuurgenzi Mkuu CPA. Hosea Kashimba, waligawa miche kwa wastaafu watarajiwa ikiwa ni mpango wa PSSSF kuunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Wakati akizindua kampeni hiyo Septemba 11, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema “Tumekuja na kampeni ya upandaji miti kwa hisani ya Mfuko wa PSSSF, tunaomba mtusaidie mtakaporudi maofisini muwaeleze wenzetu ambao ni miongoni mwa wanachama wa PSSSF, kila mfanyakazi atupandie mti mmoja uitwe PSSSF, hii itasaidia kuwa na mchango mkubwa kwa taifa letu, hatuwezi kuwa na hifadhi ya jamii huku jua likiwaka linawaka kweli kweli, linaathiri ustawi wetu, au upepo ukivuma unang’oa mabati yetu. Ni muhimu tutengeneza mazingira yetu yatakayotufanya tuishi mahali salama sisi na vizazi vijavyo.”

Hapa jijini Mbeya Mkurugenzi wa Uwekezaji PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, ambaye alimuwakilisha CPA. Kashimba alisema kupitia mpango huo, PSSSF inakusudia kuwapatia miche ya miti, wanachama wake wapatao 739,000 nchi nzima wakiwemo watumishi wa Mfuko huo.

“Pia kwa kushirikiana na watumishi wa Mfuko tutaendesha kampeni ya kuhakikisha kila mtumishi anapanda na kuitunza miche kumi ya miti, kampeni hii itaendelea hadi Disemba 2023 ambako tunatarajia tutakuwa tumepanda miche takribani million 7.” Alisema

Akizungumzia kuhusu semina hiyo Bw. Magambo alisema, PSSSF inatarajia kuwa na wastaafu 11,000 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.

Alisema Wastaafu watapatiwa mafunzo ya elimu ya uwekezaji katika masoko ya fedha, taarifa za nyaraka na utaratibu wa kufuata wakati wa kustaafu, kujiandaa kisaikolojia baada ya kutoka kwenye utumishi, umuhimu wa kutunza mazingira tunayoishi kutokana na mabadiliko ya Tabianchi, na uhalifu wa kimtandao ambao unawaathiri wastaafu wengi.

Katika nasaha zake kwa wastaafu hao watarajiwa wa PSSSF, mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera amesema, semina hizi matokeo yake yatakuwa mazuri iwapo tu wastaafu hao watarajiwa watazingatia mafunzo waliyopewa.

“Kama serikali na kama mwajiri mategemeo yetu ni kuona matokeo chanya kupitia kwenu, na mimi niseme wazi kwamba nitaanza kuwafatilia ili nione nini mnakifanya kwa maendeleo yenu, mkoa wetu na taifa letu kwa ujumla.” Alisema Mhe. Homera.

Aliwahimiza washiriki hao kuwa na namna bora na sahihi ya kutumia fedha wanazolipwa baada ya kustaafu, na ameonyesha imani yake kuwa mafunzo hayo yatakuwa suluhisho la wastaafu kutapeliwa fedha za mafao na wajanja wachache.

Ni matumaini yangu baada ya mafunzo hayo mtapata uelewa juu ya matumizi sahihi ya fedha na kuwekeza maeneo salama na yenye faida.  Ninajua fedha wanazolipwa wastaafu zikitumika vizuri zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi, kutoa ajira na pia kuongeza pato la mstaafu na taifa.” Alisema.

Mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa Mhe. Juma Homera, Mhe. Juma Homera, akizungumza na wastaafu watarajiwa wa PSSSF kwenye ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya leo Septemba 19, 2023

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo (kulia), akikabidhi mche wa Parachichi kwa mmoja wa wastaafu watarajiwa wa Mfuko huo, Bw. Thadeo Daniel Deo, Afisa Mtendaji Mtaa Mangaveta Jijini Mbeya kwenye semina ya maandalizi ya kustaafu utumishi wa umma kwenye ukumnbi wa Mkapa jijini Mbeya leo Septemba 19, 2023. Katikati ni Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi, PSSSF, Bw. Ernest Khisombi.

Baadhi ya wastaafu watarajiwa wakiwa kwenye semina hiyo leo Septemba 19, 2023

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu PSSSF, akizungumza na wastaafu watarjiwa wa mkoa wa Mbeya Septemba 19, 2023.

Semina ikiendelea

Washiriki wa semina wakipiga makofi kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera.

Washiriki wa semina wakipiga makofi kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera.

Mhe. Homera (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi, PSSSF, Bw. Ernest Khisombi.

Mkurugenzi wa Uwekzaji, PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo (wakwanza kushoto) ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, akiwa na viongozi wenzake kwneye semina hiyo.

Viongozi wa PSSSF na Ofisi ya Kazi jijini Mbeya, wakiongozwa na Meneja wa PSSSF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Ramadhan Mgaya (wakwanza kushoto) wakimpokea Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Juma Homera wakati akiwasili ukumbini.