November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu azindua mpango mkakati wa AMREF

-Asisitiza mashirika yasiyo ya kiserikali yazingatie maadili

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua Mpango Mkakati wa miaka nane wa AMREF Tanzania na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji ili kuhakikisha afua zilizopo katika mpango huo zinatekelezwa kwa ufanisi na kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mpango mkakati huo ambao unatarajia kugharimu dola la kimarekani milioni 458 kwa miaka yote nane utajikita katika kuboresha Afya ya msingi ikiwemo, kutekeleza afua za afya ya uzazi pamoja na afya ya mama na mtoto, afua za magonjwa yasiyoambukiza utasaidia katika kuimarisha afya na ustawi wa Watanzania

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 15, 2023) wakati akizindua mpango huo katika Hoteli ya Serena, Dar Es Salaam. Mpango mkakati huo kuanzia mwaka 2023 hadi 2030 ili kuelekea katika malengo ya maendeleo endelevu ya dunia 2030.

“Niwahakikishie kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya Tanzania Bara, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Afya Zanzibar, na wizara nyingine zote ambazo shughuli zenu zinahusiana nazo itaendelea kushirikiana na Amref Tanzania katika utekelezaji wa mpango mkakati huu”

Katika Hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, kuzingatia maadili ya nchi wakati wa utekelezaji wa afua mbalimbali. “Msikubali kutumika kuwa chombo cha kuhamasisha mmomonyoko wa maadili ya Taifa letu. Kila shirika litekeleze majukumu yake kwa kuzingatia mkataba uliopo kati yake na Serikali. ”

Aidha, amezitaka Mamlaka zote za Serikali zinazohusika na usajili wa mashirika yasiyo ya Kiserikali kufuatilia kwa karibu utendaji wa mashirika hayo ili kuzuia mianya ya kuhamasisha vitendo vya mmonyoko wa maadili.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta Afya na kutengeneza mazingira rafiki kwa wadau. “Leo tunaposhuhudia uzinduzi wa mpango huu haya ni matokeo ya dhamira njema ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.”

Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Mhe, Nassor Ahmed Mazrui ambaye alimuwakilisha Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa asasi zisizo za Kiserikali katika kuhakikisha zinasaidia kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi

“Tutaendelea kuweka sera na mipango madhubiti ili kufanikisha mpango kazi wenu wa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini”

Naye Mkurugenzi Mkazi wa AMREF Tanzania Dkt. Florence Temu amesema gharama za kutekeleza mpango mkakati huo itakuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2023 itakuwa ni Dola za marekani milioni 40 ambayo itakuwa ikikua kwa asilimia 30.

Amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2030 zitahitajika dola za marekani milioni 78 hivyo kufanya jumla kuu kuwa dola za marekani milioni 458 kwa miaka yote minane ya utekelezaji wa mpango huo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi la Shirika la AMREF Tanzania Anthony Chamangwana amesema kuwa Amref itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuwafikia wananchi kwa idadi kubwa zaidi na wanufaike na huduma bora za afya kuanzia ngazi ya jamii hadi ngazi ya Taifa.