November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Rwakatare aishukuru serikali kwa mazingira mazuri ya uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online Dodoma

MWENYEKITI wa Wazazi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Dk. Rose Rwakatare, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wazawa.

Ametoa shukrani hizo jana jijini Dodoma wakati wa mahafali ya kwanza ya darasa la saba shule ya Awali na Msingi ya East Africa ya mkoani Dodoma.

“Serikali ilipohamia hapa wakati wa hayati Rais Magufuli alitoa wito kwa wawekezaji kuwekeza miundombinu mbalimbali ili kusaidia kutoa elimu na sisi kama watua mabo tumebobea katika elimu tuliamua kuwekeza kwa kujenga shule hii ili kuweza kutoa elimu bora”amesema

Amesema lengo la shule ni kuunga mkono jitihada za serikali katika utoaji wa elimu bora kwa watoto wa kitanzania ili kuwawezesha kutoa ushindani katika soko la ajira duniani.

Amesema shule hiyo itaendelea kuwa shule bora kwa kuhakikisha inakuwa kwenye orodha za kuu kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa na kimkoa .

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma Pilly Mbaga, amesema kutokana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili wazazi wanatakiwa kuwalinda watoto ili wasiharibiwe na tamaduni za kigeni ikiwemo kujihusisha na vitendo vya ndoa za jinsia moja.

Mbaga, amesema hivi sasa Dunia imeharibika sana hivyo wazazi wanao wajibu wa kuhakikisha wanawalinda watoto wao ili wasiharibiwe na tamaduni za mataifa mengine.

“Hivi sasa ndugu zangu dunia imeharibika sana vitendo vya mmomonyoko wa maadili vimekithiri sana hivyo wazazi mnapaswa kuwalinda watoto ili wasiharibiwe na tamaduni za mataifa mengi.

“Mataifa ambayo yamekuwa yakihamasisha masuala ya ndoa za jinsia moja na mambo mengine ambayo ni kunyume ya tamaduni za kitanzania na nikinyume na mpango wa Mungu”amesema Mbaga

Aidha, amewataka wazazi kuacha tabia ya kutelekeza suala la malezi ya watoto kwa walimu pekee yao bali wanapaswa kuwasimamia na kuwafuatilia kila wakati ili wabaini vikwazo ambayo wanakabiliwa navyo.

“Wazazi hatupaswi kuacha suala la malezi kwa walimu pekee yao bali tuhakikishe kuwa tunawafuatilia watoto wetu kwa kushirikiana na walimu ili kuwasaidia wasiingie kwenye mikono ya shetani hali ibadilika sana hivi sasa watoto wamekuwa na tabia za ajabu ambazo kama hatutakuwa makini nao tutawapoteza”amesema

Kadhalika, amewataka walimu kuhakikisha kuwa wanasimamia watoto hasa wanapokuwa katika mabweni ili kubaini kama kuna mabadiliko yoyote ya kitabia na kuchukua hatua mapema kabla ya kundi kubwa kuharibiwa.

Vile vile, aliipongeza shule hiyo kwa kuunga mkono wa jitihada za serika katika uwekezaji kwenye sekta ya elimu ili kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.

“Mkurugenzi niwapongeze sana kwa uwekezaji huu katika sekta ya elimu sisi chama pamoja na serikali kwa ujumla tutaendelea kutoa ushirikinao kwenu ili mfikie malengo yenu”amesema

Amesema azma ya serikali ya awamu ya sita ni kuboresha elimu ambapo hivi sasa imefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa madarasa,maabara, mabweni pamoja na miundombinu mingine ili kuinua kiwango cha elimu nchini.