November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Haya ndiyo yamedhihirishwa na MkutanoTCD, Rais Samia alivyokuza demokrasia -2

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KATIKA sehemu ya kwanza ya Makala haya, tuliona jinsi uongozi wa Rais Samia Suhulu Hassan, unavyozidi kukuza demokrasia nchini, kiasi cha kumaliza malalamiko yaliyokuwa yamekithiri nchini kuhusu ukandamizaji wa demokrasia.

Kielelezo sahihi cha ukuaji wa Demokrasia nchini ni mkutano wa wadau ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wiki iliyopita, ambapo kwa mara ya kwanza yale malalamiko ambayo Rais Samia alikumbana nayo, wakati wa mkutano wake wa kwanza na wadau hao, mara hii hayakujitokeza kabisa.

Aidha, tumeona jinsi ukuaji wa demokrasia nchini unavyoungwa mkono na Balozi wa Marekani nchini, mbele wa wajumbe wa Mkutano wa TCD, Michael Battle, ambaye alisema;

“Tunasifu Tanzania kwa kupiga hatua kwenye ukuaji wa demokrasia na sisi (Marekani) tutaendelea kuiunga mkono Tanzania.”

Pia, katika sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliona jinsi Rais Samia alivyoweza kukuza demokrasia kwenye maeneo yaliyokuwa wakilalamikiwa awali ambapo aliondoa zuio la mikutano ya vyama vya siasa.

Maeneo mengine ni ya Watanzania kusahau mabomu ya Polisi, ambayo walizoea kuvurumishiwa hasa wakati wa mikutano ya siasa ya vyama vya upinzani, kufutwa kesi za wanasiasa wa upinzani na waliokimbilia nje wakihofia usalama wao.

Katika mwendelezo wa makala haya Mwandishi wetu, anaeleza maeneo mengine ambayo Rais Samia ameweza kushamirisha demokrasia ndani ya kipindi cha uongozi wake na kilio hicho hakikujitokeza tena kwenye mkutano wa TCD.

*Amerejesha uhuru wa kutoa maoni hadi unatumika vibaya

Wakati Rais Samia akiingia madarakani, alikuta kilio cha uhuru wa kutoa maoni kuminywa. Watu wengi, hususan wanasiasa wengi walifunguliwa kesi za uchochezi.

Kesi hizi, hazikuhusu wanasiasa peke yao, bali hata vyombo vya habari. Kwa miaka sita ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano, Mahakama ilionekana ni sehemu ya maisha ya kawaida ya wanasiasa.

Mfano, Uongozi wa Juu wa CHADEMA ukiongozwa Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, uliburutwa mahakamani na hatimaye viongozi hao tisa kutiwa hatiani

Mbali na Mbowe, viongozi wengine wanane wa chama hicho, wakiwemo wabunge sita walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya jinai yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Viongozi hao walikuwa ni pamoja na waliokuwa wabunge kipindi hicho, Esther Matiko; Mchungaji Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa-Zanzibar, Salum Mwalimu; John Mnyika; Halima Mdee; John Heche; Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hicho, Dkt. Vicent Mashinji.

Viongozi hao mbali na kutiwa hatiani na kutakiwa kutumikia kifungo au kulipa fani, adhabu yao iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu, ilitenguliwa na Mahakama Kuu, uamuzi uliotolewa wakati wa uongozi wa Rais Samia.

***Zitto

Aidha, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, ACT-Wazalendo, ni miongoni mwa wanasiasa waliofunguliwa na kesi yenye mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327/2018 iliyokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

***Lema, Lissu

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, ni miongoni mwa wanasiasa walioburuzwa mahakamani kutokana na kesi za uchochezi.

Kesi hizo zilivihusu hata vyombo vya habari ambavyo vililipoti yale ambayo walizungumza wakitoa maoni yao. Hii ni mifano michache, inayoonesha kwamba tuliko tuko kulikuwa kugumu kwa wanasiasa. Hii ni sehemu ya mifano michache.

Lakini tangu aingie madarakani Rais Samia, wanasiasa wanafanya kazi zao za kisiasa bila kubugudhiwa, huku wengine wakitumia lugha ngumu, ambazo sio sehemu ya utamaduni wa Watanzania, lakini wameachwa na wameendelea kufanya siasa zao.

Hii inadhihirishwa na Mkutano wa TCD, kwani hakuna aliyesimama, kulalamikia uhuru wa kutoa maoni. Sasa hivi kinachoongelewa na kutamani kiwekewe mipaka ni uhuru wa kutoa maoni, maana uhuru huo, kwa sasa inaonekana umepitiliza.

Matumizi mabaya ya Uhuru wa kuongea unatumbusha umuhimu wa maneno aliyowahi kusema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alisema;

“Uhuru wa kuzungumza upo lakini kila uhuru una mipaka yake.” Mwalimu Nyerere) alifundisha kwamba uhuru bila nidhamu ni uwendawazimu na nidhamu bila uhuru ni utumwa kwa hiyo lazima kila uhuru uwe na mipaka yake.

Lakini kwa ujumla uhuru upo wa kutosha wakati mwingine kuna kasoro katika utekelezaji wake. Nadhani Watanzania wanapiga kelele katika kusimamia sheria zinapowapa Watanzania uhuru wa kusema.

Eneo hili nalo limezidi kumpaisha Rais Samia mbele ya TCD na mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Taifa kubwa kama Marekani.

***Amerejesha Uhuru wa vyombo vya habari

Wakati Rais Samia, akiingia madarakani alikuta kilio kikubwa cha uhuru wa vyombo vya habari kuminywa. Alikuta baadhi ya magazeti, mitandao ya kijami ikiwa imezuiwa kufanyakazi zake.

Kilio kingine kilikuwa ni Sheria ya Huduma xa Habari ya Mwaka 2016, sheria hii ilikuwa na vipengele vingi, ambavyo vilikuwa vinazuia uhuru wa upashanaji habari nchini. Vifungu vingi, ilikuwa kandamizi, ambapo vilikuwa vikilalamikiwa ndani na nje ya nchi.

Ndani ya uongozi wake, Sheria hiyo imefanyiwa marekebisho hatua ambayo imepongezwa na wadau mbalimbali ikiwemo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Mazingira ya waandishi wa habari kufanyakazi yamekuwa rafiki zaidi, hatujashuhudia chombo cha habari kikivamiwa kama ambavyo tulishuhudia huko nyuma, Mfano mzuri ni yale yaliyotokea Clouds Media. Haya yote ni maeneo ambayo Rais Samia, amedhihirisha kwamba ameliongoza Taifa letu kupitia mstari mnyoofu, ndiyo maana vilio hivyo, havikusikika kwenye mkutano wa TCD.

***Kumaliza mpasuko uliokuwa ukinyelemea Taifa

Jambo lingine ambalo Rais Samia amefanya, ni kuendelea kuunganisha Watanzania kama Taifa. Ile hali iliyokuwa imeanza kujitokeza ya baadhi ya wanasiasa wa chama fulani, kumuona mwanasiasa wachama kingine adui, haipo tena.

Huko, nyuma katika baadhi ya maeneo hapa nchini Mwana-CCM alipofariki, wafuasi wa CHADEMA walipotaka kupeleka rambirambi, ilikataliwa kwa misingi ya itikadi za kisiasa.

Hili lilikuwa tishio baya ndani ya Taifa letu. Tishio hilo halipo tena, sasa hivi Rais Samia anaelekea kuzigeuzwa siasa kama mchenzo wa mpira wa miguu.

Kwenye mpira wa miguu vita ya timu mbili inakuwa ndani ya dakika 90, wakati mwingine wachezaji wanaweza kuchezeana rafu mbaya, hadi kufikia hatua ya kukunjana jenzi.

Lakini baada ya 90 kumalizika, upeana mikono na kukumbatia, kudhihirisha kwamba mpira sio vita.

Huko ndiko Rais Samia anakopeleka Taifa letu, sasa hivi wanasiasa wanaonesha kupendana, wanatofautiana kisiasa kwa hoja. Hii inadhihirishwa na kitendo cha Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM), ambaye hivi karibuni alienda kwenye mkutano wa CHADEMA, kusikiliza yaliyokuwa yakiongelewa kwenye mkutano huo.

Pengine huko nyuma, asingekuwa Rais Samia, Kishimba angekuwa amefutwa uanachana wa CCM.

Inaeledelea kesho