Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe.Hamza Hassan Juma amezindua Mwongozo wa Uandaaji na Uandishi wa Sera za Kisekta, Zanzibar – 2022 Agosti 25, 2023 katika Ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul – Wakili Kikwajuni Zanzibar.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesemea kuwa ni miongoni mwa muendelezo wa utekelezaji wa hati ya kisheria Nambari 14 ya mwaka 2020 iliyoitaka ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi kupitia Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo kusimamia masuala ya Sera za kisekta nchini.
Mhe. Hamza alisema, Ofisi yake imechukua jitihada mbali mbali za kuifanyia kazi hati hiyo ya kisheria ikiwemo kufanya tathmini ya Utekelezaji wa Sera za Serikali ambapo tathmini ya kina kwa Sera 39 ilifanyika na mambo mbalimbali yalibainika yakiwemo mapungufu, mafanikio na changamoto zilizopo katika kusimamia uratibu wa uandaaji na utekelezaji wa Sera nchini.
“Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni kutokulingana kwa miundo ya kisera nchini jambo ambalo linaweza kurejesha nyuma upatikanaji halisi wa utekelezaji wa Sera.Aidha, kupitia Ripoti ya Tathmini hiyo pamoja na mambo mengine Ofisi yangu imeandaa Mwongozo huu ambao utakuwa umetatua changamoto mbali mbali na utaleta matarajio mazuri katika uratibu wa Sera nchini kwa maslahi ya nchi yetu,” alisema Mhe. Hamza
Ameongezea kuwa Mwongozo umezingatia miongozo ya Kikanda na Kimataifa, Ilani ya Uchaguzi 2020 – 2025 na Mipango ya Maendeleo Endelevu ya Kitaifa na Kimataifa.
“Ofisi inaimani kikao hichi chenye ushiriki wa Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi, Wakuu wa Mashirika, Wakurugenzi, Wakuu wa Vyuo, Sekta Binafsi na Maafisa Viungo wanaosimamia Sera ni ishara njema inayoonesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyojali ushirikishwaji wa Taasisi za Umma na za Binafsi katika kusimamia maendeleo ya nchi hii,” alieleza.
Aidha, uzinduzi ulihusisha wajumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni ishara na kielelezo cha Muungano wetu kuhakikisha inaendeleza mashirikiano hasa katika Sera zinazotekelezwa katika pande zote mbili za Muungano kwa kuwa na mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa Sera zenye sura ya Muungano.
Ametoa wito kwa Wizara zote kutoa elimu stahiki ya Sera zao na kuandaa utaratibu wa ushirikishwaji wa wadau husika katika uandaaji na utekelezaji wa Sera hizo sambamba na kuufanyia kazi mwongozo huu kwa manufaa ya umma.
“Ni muhimu kuzingatia suala zima la kuzifanyia mapitio Sera zote ambazo zinaonekana zimepitwa na wakati kwa kuzingatia taratibu zilizoainishwa kwenye mwongozo huu,” alisisitiza Mhe. Hamza
Akitoa salamu za Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Katibu Mkuu ofisi hiyo anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa amesema uwepo wa Mwongozo utaongeza tija na matokeo chanya katika sekta mbalimbali katika kutoa huduma kwa jamii huku akieleza kuwa, ofisi yake itaendelea kuimarisha mashirikiano na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi hususan katika kuratibu masuala ya sera nchini.
“Tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano pamoja na kujifunza kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hususan Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika maeneo yote yanayoratibiwa na Serikali hizi mbili,” alisisitiza
Mutatembwa aliongezea kuwa uwepo wa mwongozo huu utaimarisha utekelezaji wa Sera kwa kuwezesha kuwa na sera zilizoandaliwa kwa kuzingatia Sera shirikishi na kuakisi hali halisi.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa