Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
Serikali imewataka Wadau mbalimbali kuendelea kupambana dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini kwa kuunganisha nguvu hasa kushirikiana na Serikali kutoa elimu kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kikao cha kuwapongeza na kutoa tuzo kwa Wadau na mabalozi waliowezesha uzinduzi wa Kampeni ya Zijue Fursa Imarisha Uchumi Kataa Ukatili Kazi Iendelee (ZIFIUKUKI).
Waziri Dkt. Gwajima amesema Katika kutimiza azma hiyo, Wizara inashirikiana na Wadau kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu kudhibiti vitendo vya ukatili kwa ustawi na Maendeleo ya Taifa letu.
Ameongeza kuwa Tamasha la Maendeleo lililofanyika utarehe 27 hadi 29 Aprili, 2023 katika Viwanja vya Leaders Club Kinondoni Jijini Dar es Salaam lilienda sambamba na utoaji elimu na huduma mbalimbali za kijamii, huku wananchi Elfu Kumi na Sita (16,000) walihudhuria Tamasha na jumla ya watu Elfu Nne na Arobaini (4,040) walipatiwa huduma muhimu hasa elimu ya kupambana na ukatili.
“Ninawashukuru sana kwa huduma mbalimbali za kijamii mlizotoa kwa wananchi waliohudhuria katika uzinduzi wa tamasha hilo. Hivyo kukutana nanyi hapa leo ni kwa lengo moja tu; kuwashukuru kwa ushiriki na mchango wenu uliowezesha Wizara kufanikisha uzinduzi wa Tamasha hilo” amesema Waziri Dkt. Gwajima
Aidha amesema kuwa Wizara inaendelea na maandalizi kwa ajili ya matamasha ngazi ya Mikoa na kusisitiza kuwa Wizara inatambua matamasha yana nguvu ya kipekee katika kuifikia jamii hivyo amewapongeza walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha uzinduzi wa tamasha la maendeleo la ZIFIUKUKI.
“Wizara itaendelea kushirikiana nanyi katika kuhakikisha tunakuza fursa za kiuchumi kwa wananchi na kutokomeza ukatili hapa nchini” alisema Waziri Dkt. Gwajima
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Juliana Kibonde amesema Idara kupitia Wizara itaendelea kushirikiana na wadau na mabalozi katika kuhakikisha elimu ya kupinga ukatili, malezi na Makuzi ya Mtoto, usawa wa kijinsia na Maendeleo ya Ustawi wa Jamii kiujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya FAGDI iliyosimamia maandalizi ya Tamasha hilo kwa kushirikiana na Wizara, ambaye pia ni Msanii wa Bongo Filamu nchini Simon Mwapagata amesema wakiwa ni vijana wa kitanzania wataendelea kuibeba Kampeni hiyo hasa katika kutoa elimu kuhusu maadili kwa Vijana ili kuwa Taifa lenye maendeleo na Ustawi mzuri.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake