Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
MTENDAJI Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Mussa Budeba amesema uwepo wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi wa sampuli za madini, uchenjuaji, utambuzi wa tabia za miamba na wataalam wenye weledi, umevutia wateja kutoka miradi mikubwa ikiwemo ya Kimani, Bwawa la Umeme la Julius Nyerere na Mgodi wa Dhahabu wa Geita kutumia maabara hiyo.
Dkt. Budeba ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya maabara ya taasisi hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Agosti 24, 2023 jijini Dodoma ambapo pia, Kamati hiyo imepata fursa ya kutembelea maabara hizo zilizopo eneo la Mbwanga kujionea namna shughuli za upimaji, uchenjuaji na utambuzi wa madini zinavyofanyika.
Amesema kutokana na ubora wa vifaa imepelekea ongezeko la wateja na sampuli za uchunguzi na hivyo kuwa kichocheo kikubwa cha kuongeza makusanyo ya ndani ambapo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 Kurugenzi ya Maabara ilichunguza sampuli 22,343 na kuvuka lengo la mwaka la kuchunguza sampuli 17,000.
Pia, ameongeza kwamba, ufanisi wa vifaa umepelekea kuzalisha vyungu vya kuyeyushia sampuli za dhahabu (crucibles) vyenye ubora na vinavyokidhi mahitaji ya wateja ikiwemo kupunguza malalamiko ya wateja yaliyotokana na utambuzi wa madini ya vito.
‘’ Mhe. Mwenyekiti, vifaa vipya vya maabara vimeongeza wigo wa watafiti, wahadhiri na wanafunzi wa shahada ya kwanza, pili na tatu kutokaVyo vikuu vya Dar Es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Mtakatifu Yohana na vingine kuitumia maabara ya GST.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kamati kutembelea maabara hizo, Dkt. Budeba amesema mikakati ya taasisi hiyo ni kuboresha maabara zilizo pembezoni na kupeleka huduma za maabara katika maeneo mbalimbali nchini na kueleza kuwa, kwa kuanzia, tayari imeanzisha maabara ya upimaji sampuli katika Mkoa wa Geita na mpango wa sasa ni kuanzisha maabara Wilayani Chunya huku mkakati iliyopo ni kuwa na maabara kwenye kanda mbalimbali nchini.
‘’ Mikakati yetu mingine ni kuanza kufanya tafiti za mbolea, GST ipo kwa ajili ya watanzania hivyo tunawakaribisha wachimbaji kuzitumia maabara zetu pamoja na kupata machapisho mbalimbali yanayoonesha uwepo wa madini yetu katika mikoa mbalimbali nchini, hii itawasaidia wachimbaji kuchimba bila kubahatisha, kuongeza mapato na kupunguza utegemezi kutoka Serikalini, ‘’ amesisitiza Dkt. Budeba.
Akizungumza baada ya kutembelea maabara hizo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Judith Kapinga amesema kamati hiyo imetembelea kuona uwekezaji huo uliofanywa na Serikali ambapo bunge liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 4.2 na hadi sasa tayari GST imetumia shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
Ameongeza kwamba, vifaa hivyo vinatarajia kuongeza tija katika shughuli za utafiti na uchenjuaji madini na kuipongeza kwa kujiongeza kutafuta miradi ya kuongeza mapato ya taasisi kupitia mradi wa uzalishaji vyungu vya kupima sampuli za dhahabu.
Aidha, kutokana na umuhimu wa taasisi hiyo kwa maendeleo ya Sekta ya Madini, amesema kamati itaendelea kuishauri Serikali kuongeza bajeti ya kuwezesha shughuli za GST pamoja na kuboresha miundombinu.
Katika michango wa wabunge, wameishauri GST kuongeza kasi katika kuzalisha vyungu vya aina mbalimbali vya kuchomea dhahabu kutokana na mahitaji yaliyopo pamoja na kuongeza wigo wa kufanya tafiti.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili