Na Allan Vicent, TimesMajira Online, TaboraWAZAZI na walezi Wilayani Sikonge Mkoani Tabora wametakiwa kuhakikisha watoto wao wa kiume na kike waliofikia umri wa kwenda shule wanapelekwa ili kupata elimu itakayowawezesha kuwa wataalamu wa fani mbalimbali.Wito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Halima Mamuya alipokuwa akiongea kwa nyakati tofauti na wakazi wa Vijiji vya Msuva na Ugunga katika kata za Ngoywa na Ipole Wilayani humo.Alisema baadhi ya wazazi na walezi wanaoishi vijijini wamekuwa wakizuia watoto wao kwenda shule huku wanaume wakitumikishwa katika shughuli za kilimo au kuchunga ng’ombe na wale wa kike wakilazimishwa kuolewa.Mamuya alisisitiza kuwa kumzuia mtoto kupata elimu ni kumnyima haki yake ya msingi na kumfanya ashindwe kutimiza ndoto za maisha yake, hivyo akawataka kubadilika na kuwaacha wasome ili kuongeza idadi ya wataalamu.‘Wazazi na walezi pelekeni watoto wenu shule, serikali inahitaji wataalamu wengi zaidi katika fani mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, barabara na nyinginezo,  sasa wasipopelekwa tutapata wapi wataalamu’, alisema Mhesh Mamuya.Alibainisha kuwa hivi karibuni serikali imetoa kiasi cha milioni 234 ili kufanikisha ujenzi wa vyumba 8 vipya vya madarasa katika shule ya msingi Kininga wilaya ya Sikonge na mradi uko katika hatua za mwisho kukamilika hivyo akahoji wasipopelekwa shule wataalamu watapatikana wapi.‘Wakulima na wafugaji badilikeni, acheni watoto wenu wasome ili mpate wataalamu watakaowasaidia kulima na kufuga kisasa na kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo’, alisema.Diwani wa Kata ya Ngoywa Leonard Kwilasa alithibitisha kuwepo baadhi ya wazazi wenye tabia za namna hiyo hususani wanaoishi vijijini hivyo akamhakikishia kuwa watawasaka na kuchukua hatua stahiki ikiwemo kulipa faini.Alisema baadhi ya watoto wamekuwa wakishindwa kuendelea na shule kutokana na wingi wa michango mashuleni ambayo hupelekea baadhi ya wazazi kushindwa kuwalipia watoto wao hivyo kuwaacha tu wakae nyumbani.Katika kutatua suala hilo Mjumbe wa Kamati Kuu Mamuya alishauri Kamati za Shule zote kukaa na wazazi na walezi ili kuangalia namna ya kupunguza gharama za michango ili kuwaondolea mzigo huo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa