Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa kuzingatia maadili na nidhamu katika maeneo ya kazi ili kuwa picha nzuri na ya mfano kwa wengine.
Makamu wa Rais amesema hayo leo Tarehe 22 Agosti 2023 wakati akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliopo Kibaha Mkoani Pwani. Amesema ni lazima wakati wote wa uongozi kutafuta njia bora ya kuwashirikisha wengine ili msingi wa uongozi na utendaji uwe chachu zaidi kuleta maendeleo kwa wananchi.
Pia Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mikoa kuongeza jitihada kuiwezesha sekta binafsi ili iweze kukua, kushamiri na kuzalisha ajira kwa kuweka vivutio na mazingira mazuri ya uwekezaji. Amesema sekta binafsi inapaswa kuwa mshirika muhimu katika shughuli zote za maendeleo katika mikoa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema maudhui ya mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo yanalenga kuondoa matukio mbalimbali yanayotokana na mapungufu katika uongozi ikiwemo kutokuzingatia mipaka ya kiutendaji kati ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wao hususan katika matumizi ya fedha pamoja na kushindwa kudhibiti uvujaji wa siri za Serikali hususan katika zama hizi za utandawazi na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala kuzingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira hususani kutunza vyanzo vya maji, kufuatilia fursa mbalimbali zitokanazo na shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na biashara ya Kaboni na Uchumi wa Buluu. Amewataka kuhakikisha kunakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuepuka migogoro mbalimbali ndani ya jamii na kuzingatia changamoto zozote zinazojitokeza katika jamii zinashughulikiwa mapema na kwa ukamilifu.
Makamu wa Rais amesema dhima ya mafunzo hayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020, ambayo inaelekeza umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika hali iliyo shirikishi na yenye ubora. Ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa mafunzo hayo muhimu kwa viongozi
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Angellah Kairuki amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea viongozi hao uwezo wa kuongoza na kusimamia wananchi, fedha na rasilimali zingine muhimu za taifa. Pia amesema mafunzo hayo yatawawezesha viongozi kuwa na maamuzi ya kimkakati pamoja na kuwawezesha kuwa na uwezo katika masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao.
Ameongeza kwamba katika siku sita za mafunzo jumla ya mada 20 zinatarajiwa kuwasilishwa kwa viongozi hao ambazo zitajikita katika masuala ya uongozi, usimamizi rasilimali, miongozo na taratibu mbalimbali za utendaji kazi serikalini, usimamizi miradi na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kukuza uchumi.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili