November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sh.6.7 Trilioni zahitajika kufikisha umeme Vitongoji 36,101

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI kupitia Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) imesema,vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na miundombinu ya umeme nchini ni 36,101 kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo Tanzania Bara huku akisema sh.Trilioni 6.7 zinahitajika kufikisha umeme katika vitongoji hivyo vilivyobaki.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuuwa REA Mhandisi Hassan Saidy wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majuku ya taasisi hiyo kwa mwaka 2023/24.

Aidha Saddy amesema,Serikali ilipata mkopo wa gharama nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo kiasi cha shilingi bilioni 100 zitatumika kuanza utekelezaji wa mradi huo katika vitongoji 654 katika mikoa ya Songwe na Kigoma na hivyo kufanya vitongoji ambavyo havina umeme kubaki 36,101. 

“Mradi wa Ujazilizi Mzunguko wa Pili B unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vitongoji 1,686 katika mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Morogoro, Njombe na Songwe na kuunganisha jumla ya wateja wa awali 95,334,gharama a mradi huo ni sh.234.4 bilioni.”amesema Saddy na kuongeza kuwa

“Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Mradi wa Ujazilizi Mzunguko wa Pili C unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vitongoji 1,880 katika mikoa ya Manyara, Iringa, Rukwa, Mtwara, Ruvuma, Simiyu na Mara kwa kujenga kilomita 6,562 za msongo mdogo na kufunga mashineumba 1,932 ili  kuunganisha wateja wa awali 131,719. “

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo gharama ya mradi huo ni shilingi bilioni 293 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali za Norway na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Aidha amebainisha kuwa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme ifakara (220/33kv, 1x20mva) na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme unahusisha ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara na Ujenzi wa Njia ya Kusambaza Umeme Vijijini (Wilaya za Kilombero na Ulanga). 

Amesema,mradi unalenga kuwezesha na kuimarisha shughuli za kilimo katika eneo la SAGCOT kwa kuwapatia wananchi huduma za umeme ambapo gharama za mradi ni shilingi bilioni 23.62 ambazo zinalipwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya.

“Mradi huu utawezesha wateja wapatao 1,853 kuunganishiwa umeme katika vijiji nane na vitongoji saba.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema kuwa Serikali kupitia REA, imewapata waendelezaji watatu wa miradi ya kusambaza umeme kwa kutumia nguvu ya jua, itakayotekelezwa katika visiwa 28 vilivyopo katika mikoa ya Kagera (8), Mwanza (13), Mara (3) na Lindi (4) na hivyo kuunganisha wateja 9,515 kwa gharama ya shilingi bilioni 11.18. 

Pia amesema,REA inatekeleza mradi wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za petroli vijijini kwa njia ya mkopo nafuu unahusu kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za mafuta katika maeneo mbalimbali ya vijijini ambapo mradi wa utoaji Mikopo ya Ujenzi na Uendeshaji wa Vituo Vidogo vya mafuta ya Petroli na Diseli vijijini Tanzania bara utatolewa.

“Malengo makuu ya mradi huo ni kulinda mazingira na afya ya watumiaji na kuboresha upatikanaji na usambazaji wa mafuta vijijini ambao kiasi cha mwisho cha mkopo ni shilingi milioni 75 na kiasi cha riba ni 5% huku muda wa marejesho ukiwa ni Miaka 7.amesema na kuongeza kuwa

“Katika Mwaka wa Fedha 2023/24, kiasi cha shilingi bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu kwa waendelezaji, kwa sasa, Wakala unaendelea kupokea maombi ya waombaji na mwisho wa kupokea maombi hayo ni 25 Agosti 2023.”

Akizungumza kuhusu  mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG), Wakala umeanza kutekeleza mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000 yenye thamani ya shilingi bilioni 3 pamoja na majiko banifu 200,000 katika maeneo ya vijijini.

Amebainisha kuwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, jumla ya fedha takribani shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi huo.