Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa Tabora wametoa tamko la pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuimwagia mabilioni ya fedha Halmashauri hiyo ili kufanikisha utekelezaji miradi ya kimkakati.
Akitoa tamko hilo kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ramadhan Kapela, Diwani wa Kata ya Mwinyi, Mwalimu Nasri Mnenge amesema Rais amegusa mioyo ya wakazi ya Manispaa hiyo kwa kuwapatia zaidi ya sh bil 12 ili kutekeleza miradi yenye maslahi mapana kwa wananchi.
Amebainisha kuwa Rais ana dhamira njema ya kuinua maisha ya wananchi ndiyo maana ameendelea kupeleka fedha nyingi katika halmashauri zote nchini ikiwemo Manispaa hiyo ili kuhakikisha huduma bora za kijamii zinapatikana wakati wote.
Alitaja baadhi ya sekta ambazo zimepokea fedha katika Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji miradi ya kimkakati kuwa ni elimu, maji, afya na miundombinu ya barabara.
Mnenge amebainisha kuwa hivi karibuni tu wamepokea kiasi cha sh bil 1.8 kwa ajili ya miradi ya elimu lengo likiwa kuifanyia maboresho makubwa miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika manispaa hiyo.
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia pia ametoa kiasi cha sh bil 2.2 kwa ajili ya kuboreshwa shughuli za kilimo katika manispaa hiyo lengo likiwa kuinua maisha ya wakulima waliopo katika halmashauri hiyo.
Aidha Mnenge amebainisha kuwa pia wamepokea kiasi cha sh bil 4.3 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji la Magoweko ili kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara .
Kwa upande wake Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Rose Kilimba amewataka madiwani wenzake kusimamia ipasavyo miradi inayotekelezwa katika kata zao ili thamani ya fedha hizo ionekane na wananchi wanufaike.
Aidha amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Elias Kayandabila na wasaidizi wake katika usimamizi wa fedha hizo na kumtaka kutofumbia macho uzembe wowote katika miradi hiyo.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora Mjini Neema Lunga amesema chama kinaridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais na kubainisha wazi kuwa ilani ya uchaguzi imetekelezwa kwa vitendo.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â