Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
ZAIDI ya sh bil 2.4 zinatarajiwa kukusanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani hapa kutokana na ushuru wa mauzo ya zao hilo katika msimu wa 2022/2023 baada ya juhudi za serikali kufanikiwa kuongeza wanunuzi wa zao hilo.
Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Said Ntahondi alipokuwa akifungua kikao cha baraza la madiwani ambapo alisema kiasi hicho kinatokana na mauzo ya kilo mil 14.8 za zao hilo kwa wastani ya Dolla 2.3 kwa kilo.
 Ntahodi alisema katika msimu huu walilenga kuzalisha kilo mil 15.05 na jumla ya kampuni 5 zilihusika kununua zao hilo na hadi masoko yanafungwa Julai 17, 2023 kilo mil 14.8 zilinunuliwa kwa thamani ya dola za kimarekani mil 34.04.
Alibainisha kuwa ongezeko la makusanyo hayo limetokana na halmashauri hiyo kuunda kikosi kazi kilichojumuhisha watendaji, madiwani na wataalamu ambacho kilifanya kazi ya kusimamia masoko hayo kwa siku zote 58.
Alisema kazi kubwa ya kikosi hicho ilikuwa kudhibiti utoroshashi wa tumbaku, kuhakikisha uhai wa vyama vya msingi (amcos) na kufuatilia mikopo na madeni ya kila mkulima ili kila mmoja apate stahiki halali na sio kupunjwa.
‘Msimu huu tulikadiria kukusanya kiasi cha sh bil1.2 tu kama ushuru wa zao hilo lakini kutokana na mikakati mizuri tuliyojiwekea ikiwemo usimamizi tunatarajia kukusanya zaidi ya sh bil 2.4,’ alisema Ntahodi.
Alibainisha kuwa mapato hayo ni mara mbili ya ya makusanyo ya misimu 2 iliyopita ambapo mwaka 2020/2021 halmashauri ilikusanya kiasi cha sh mil 565.3 kama ushuru na 2021/2022 ikakusanya sh mil 787.3.
Ntahondi alifafanua kuwa miaka ya hivi karibuni zao hilo lilipoteza mvuto kwa wakulima kutokana na kukosa soko la uhakika hali iliyopelekea wakulima wengi kupata mavuno hafifu hivyo kupunguza juhudi zao.
Alisisitiza kuwa kwa kuliona hilo serikali ililazimika kuhamasisha kampuni za ununuzi kujitokeza kwa wingi hivyo kuongezeka kutoka 2 hadi 5 na kushawishi taasisi za kifedha kuwakopesha mitaji ili waweze kupata pembejeo kwa urahisi.
Kutokana na mkazo huo wa serikali ya awamu ya sita kwenye kilimo cha zao hilo, wakulima wameweza kuongeza uzalishaji na vyama vya msingi wilayanu humo kuongezeka kutoka 54 hadi 85.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â