Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
DIWANI wa kata ya Ifucha katika halmashauri ya manispaa Tabora Bi.Rose Kilimba (CCM) ameibuka kidedea katika nafasi ya Naibu Mstahiki Meya baada ya kupata ushindi wa kishindo wa kura 33 za madiwani wote kati ya 34 zilizopigwa.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Elias Kayandabila, Afisa Utumishi Gudu Malulu alisema Rose amepata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 97.
Alisema ushindi huo ni ishara ya kuungwa mkono na madiwani wote wa kiume na kike wakiwemo wa upinzani hivyo akaomba wampe ushirikiano ili kufanikisha utekelezaji majukumu yake katika nafasi hiyo.
Aidha alimhakikishia kuwa Ofisi ya Mkurugenzi na watumishi wote wa halmashauri manispaa hiyo watampa ushirikiano unaostahili wakati wote atakapokuwa akitumikia nafasi hiyo kama walivyofanya kwa watangulizi wake.
Mwenyekiti wa kikao hicho Naibu Mstahiki Meya aliyemaliza muda wake Nasiri Mnenge (diwani wa kata ya Mwinyi) alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuteua mama jasiri na mwenye uwezo kugombea nafasi hiyo.
Alisema chama kimeteua mtu sahihi ndiyo maana ameungwa mkono na takribani madiwani wote akiwemo wa CHADEMA hivyo akaahidi kumpa ushirikiano uliotukuka.
Aliongeza kuwa ushindi huo umetokana na utendaji wake mzuri katika kata yake na ndani ya baraza hilo, ikiwemo ufuatiliaji wa karibu wa miradi inayotekelezwa na halmashauri hiyo katika vijiji na kata mbalimbali.
Akitoa salamu za chama katika kikao hicho Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tabora mjini Neema Lunga alimpongeza kwa kuaminiwa na madiwani wenzake wote na kumtaka kushirikiana nao.
Aidha alibainisha kuwa chama kinaunga mkono juhudi zote zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hivyo akaomba madiwani, viongozi wa chama na watumishi wa umma wote kuendelea kumsemea Mheshimiwa Rais.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa