December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apongezwa kwa bilioni 230/- za mwendokasi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

RAIS, Dkt Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa kutoa sh. bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya mabasi ya mwendokasi ‘BRT’ awamu ya tatu pamoja na vituo vyake yenye urefu wa kilometa 23.3.

Mradi huo ambao umeanzia Posta ya Zamani kwenda Gongo la Mboto, umepangwa kukamilika kwa ndani ya miezi 20 na hadi sasa umeishatumia miezi 11 na hivyo kutarajiwa kukamilika Mei, mwakani.

Ujenzi wa barabara hiyo imepelekea upatikanaji wa ajira kwa vijana 94 wenye vibendera ambao wanahakikisha usalama wa barabara wakati wa ujenzi masaa 24.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema barabara hiyo ni ya umuhimu, kwani inaenda uwanja wa ndege na maeneo mengi ambayo kuna wananchi wengi.

“Namshukuru Rais, Dkt. Samia, kwa kutuwezesha kuhakikisha tunajenga barabara hii ya BRT 3 ambayo ni muhimu sana kwa sababu ni barabara inayokwenda Uwanja wa Ndege na maeneo mengi ambayo kuna wananchi wengi,” alisema.

“Barabara hii ni muhimu sana katika uchumi wa nchi, hivyo Rais, Dkt. Samia alitoa takribani sh. bilioni 230 kwa ajili ya kujenga kilometa 23.3 pamoja na vituo vyake, barabara ambayo ni ya zege na inajengwa ili idumu muda mrefu.”

Aidha Waziri Prof. Mbarawa aliwataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha ujenzi ili kumpa nafasi mkandarasi aweze kujenga Barabara hiyo kwa kiwango cha juu na kusimamia usalama wa barabara hiyo.

Prof. Mbarawa aliwataka mshauri kwenye mradi huo kusimamia barabara hiyo pamoja kwa kushirikiana na TANROADS, ili ijengwe kwa viwango vinavyostahili.

Meneja Mradi BRT 3, Mhandisi Frank Mbilinyi, alisema wamejipanga ipasavyo kusimamia usalama barabarani kwa kufanya kazi pamoja na askari wa usalama barabarani.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilala, Charangwa Seleman alisema mradi huo ni muhimu kwa Wilaya ya Ilala, hivyo alimshukuru Rais, Dkt. Samia kwa kuleta mradi huo wa BRT 3 na kuwaomba wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili iweze kuwahudumia wananchi.

Katibu Tawala Wilaya ya Temeke, Nicodemus Tambo, alimshukuru Rais Samia kwa mradi huo.