Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amepokea Hati za Utambulisho za Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Elke Wisch katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri Tax amemweleza Elke Wisch kuwa UNICEF imekuwa na mchango mkubwa kuiunga mkono Serikali kwa kukuza, kulinda na kutimiza haki za watoto.
“UNICEF ni wadau wakubwa na wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika maeneno mengi na madhumuni yake ni kulinda haki ya mtoto na katika hili ni wadau wetu katika sekta za afya na elimu pamoja kuangalia maendeleo ya watoto,” amesema Dkt. Tax.
Waziri Tax ameongeza kuwa UNICEF wamekuwa pia wakisaidia katika kuhakikisha vifo vya watoto wadogo nchini vinapungua na wamekuwa na msaada mkubwa katika hilo.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi UNICEF nchini, Elke Wisch amesema kuwa UNICEF itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa na kuimarishwa kuanzia katika ngazi ya jamii na Tanzania nzima kwa ujumla.
“UNICEF tunaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa na kuimarishwa kuanzia katika ngazi ya jamii na Tanzania nzima kwa ujumla.” amesema WischAidha
Wisch ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha vizuri Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali watu (Africa Heads of States Human Capital Summit) ulifanyika mwezi Julai.
Ambapo amesema mkutano huo ulikuwa njia sahihi ya kujadili misingi ya ushirikiano pamoja na masuala mbalilmbali ya Watoto na vijana ambao ndiyo rasimali za kukuza na kuendeleza maendelea ya nchi.
Katika tukio jingine, Waziri Tax amemuaga Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Christine Musisi baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini.
Musisi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya tangu alipoinga madarakani licha ya kuingia madarakani katika kipindi kigumu cha janga la Uviko 19.
“Nimekuwa na wakati mzuri kuona nchi ikikuwa, ikiwa na ustahimilivu hata katika kipindi cha janga la Uviko 19, nimeona pia maendeleo ya watu yakiwa imara kutokana na uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wanalindwa,” alisema Musisi
Musisi ameongeza kuwa ilikuwa faraja kubwa kufanya kazi Tanzania kama mwakilishi mkazi wa UNDP ambapo alishirikiana vyema na Serikali katika kuhakikisha kuwa mpango wa maendeleo wa miaka mitano na malengo ya milenia yanatekelezwa na kutimia kama ilivyopangwa.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja