Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ametembelea kikundi cha wauzaji wa mchele (Mbeya Rice Group) katika Kongano la wauzaji mchele soko la Mwanjelwa jijini Mbeya huku akiwaeleza wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kuwa serikali itaendelea kuona na kupunguza tozo zisizo na tija kwao na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ya Kigahe imekuja kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara wa mchele katrika soko hilo la mchele kutozwa tozo nyingi na hivyo kusababisha bidhaa ya mchele kuuzwa kwa bei ghali.
“Naomba niwahakikishie kuwa serikali itandelea kuwaunga mkono katika shughuli zenu na ndiyo maana leo nimekuja nione kazi zenu lakini pia kusikia changamoto zinazokwamisha shughuli zenu ili tuweze kuzifanyia kazi.”amesema Kigahe
Aidha amewataka viongozi wa soko hilo waendelee kuboresha mchele wao ili kuhakikisha unakuwa ni bidhaa bora ambayo inaweza kushindanishwa katika soko la Kimataifa.
“Naomba mjitahidi sana katika uandaaji wa mpunga wakati mnapoelekea kuuchakata ili kupata mchele,hakikisheni mnaanika vizuri mahali ambapo hapawezi kusababisha mchele kuwa na mchanga lakini pia mtafute mashine ambayo inayoweza kupumbua mchele na chenga,lengo kubwa hapa ni kifaya bidhaa yetu ishindane kimataifa.”amesema Kigahe
Aidha amesema,Serikali inaendelea kuongea na taasisi za kifedha na hasa kwenye vikundi ili wafanyabaishara hao waweze kukopesheka na benki mbalimbali ikiwemo b enki ya TIB.
“TIB wana fedha za kutosha na wanalenga vikundi vilivyopo kwenye sekta hii ya kilimo na riba yao haizidi asilimia nane ,na mngekuwa na SACCOs yenu mngekopa kwa asilimia nne mpaka tano ,sasa hii ingewawezesha kupata mitaji na hivyo kupata teknolojia mnazozihitaji kutoka katika kiwanda cha SIDO.
Ametumia nafasi hiyo kuitaka SIDO iwapeleke TIB kuwatambulisha kwamba ni kikundi chenye tija katika uchumi wa nchi ili waaminike na kuwawezesha kupata mitaji na huduma nyingine zitakazosaidia kuboresha biashara zao.
Vile Vileameielekeza SIDO iwasaidie kutengeneza teknolojia wananzohitaji kwa gharama nafuu au iwaunganishe na sehemu ambako ni sahihi ili waweze kupata hizo teknolojia
“Kwa hiyo mimi niseme sisi tutaendelea kuwasaidia,kuwatengenezea mazingira mazuri zaidi ili mzalishe kwa tija .”
Kuhusiana na suala la ushuru mkubwa lililolalamikiwa na wafanyabiashara hao,Naibu Waziri huyo ameiagiza Ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa ilichukue hilo na waone namna ya kuangalia kupunguza ushuru ili waweze kuchukua wafanyabiashara wengi zaidi na kupata fedha nyingi licha ya kukusanya kidogo kidogo lakini itaongeza uhiyari wa kulipa kodi na hivyo serikali kupata mapato mengi zaidi.
“Kwa hiyo nadhani hili tuliangalie kama serikali na hasa wenzetu wa halmashauri mtusaidie, kwa hiyo mtaangalia maeneo ya kodi na vibali mbalimbali wanapoenda kununua mazao kwa wakulima.”amesisitiza
Awali Katibu Mkuu wa Mbeya Rice Group Julius Ngalawa amesema,lichaya changamoto wanazokumbana nazo lakini wameendelea na biashara hiyo ambayo imeajiri zaidi ya watu 3000.
“Mbeya Rice Group,tunachakata tani 78,000 za mpunga.. ,na inashughulika na mnyororo wa thamani wa zao la mpunga wanaanza kwa mkulima mpaka kwa mlaji ,tuna vikundi vya wakulima katika maeneo mbalimbali tunafanya mikataba nao na pia tuna wakulima mmoja mmoja ambao ni binafsi wanakuja kukoboa,
“Pia Mbeya Rice Group tuna watu zaidi ya 3000 tunaofanya nao kazi ambao tumewaweka katika vikundi,kuna vikundi vya washushaji ,wabeba mchele,usaidizi mashineni,pia kuna wananwake wapatao wanane wanaomiliki mitambo ya kukobolea mpunga.”
Aidha amesema ,kikundi hicho kinajishughulisha na uuzaji wa mchele nje ya nchi ambapo amesema biashara bado haiajwa rasmi lakini mpango wao ni kuhakikisha biashara hiyo inakuwa rasmi ili waweze kulipa kodi za serikali maslahi mapana ya nchi.
Amesema masoko ya mchele wanaouzalisha yapo katika nchi za Uganda,Zambia ,Botswana ,kwa hiyo Mbeya Rice Group tukajiongeza tukaona ni nafuu sasa tuwe na sehemu ambayo ni Packaging process ambayo tutakuwa tutatoa mchele katika mashine zetu tunauweka sehemu tunafanya ‘packaging’ tunaukatia vibali na kuusafirisha kwa njia halali ili serikali na wananchi kwa ujumla kila mmoja apate pato lake.
Kwa mujibu wa Ngalawa kikundi hicho kimeingia makubaliano na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH ambapo walifanikiwa kupata wazo bunifu la mashine ya kukaushia mpunga na wamepata milioni 40 kutoka COSTECH kwa ajii ya kutengenezewa mashine ya kukaushia mpunga ambayo itakuwa ni suluhisho la ukaushaji wa mpunga na kutoa bidhaa bora ya mchele.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa Mchele Joyce Mahenge amemuomba Naibu Waziri huyo awasaidie katika kupunguza utiriri wa kodi unaosababisha kuleta kero kwao na mchele kuuzwa kwa bei ghali.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja