Na Jackline Martin, TimesMajira Online
SERIKLI chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na juhudi za kurahisisha mazingira bora ya uwekezaji ambayo yameiwezesha Taasisi ya UTT AMIS kuvuka malengo ya ukuaji wa mfuko kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo vijana.
Kampuni hiyo ya UTT AMIS imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka ukubwa wa sh. bilioni 996 hadi sh. trilioni 1.535 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 54.
Aidha kwa mwaka 2022 taasisi hiyo ilikuwa na ukuaji wa asilimia 50 kutokana na ukuaji wa sh. bilioni 600- 996.
Hayo yalisemwa jana Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uwekezaji UTT AMIS, Simon Migangala, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari nchini ulioratibiwa na ofisi ya msajili wa hazina kwa lengo la kufahamisha wananchi juu ya kazi ambazo taasisi za umma zinafanya.
“Namshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuboresha mazingira, kwani katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake tumekuwa na uwekezaji mkubwa hii inaenda sambamba na ongezeko la wawekezaji na wawekezaji wengi ambao wanaingia kwenye mifuko hii wakiwemo vijana,” alisema.
Aidha Migangala alisema kwa miaka mitatu iliyopita wamekuwa na ukuaji ambao ni takribani asilimia 50, ikiwa ni ukuaji mzuri sana na umeenda vizuri pamoja na faida nzuri inayopatikana kwa wawekezaji katika mifuko yote ya UTT AMIS.
Alisema kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2023 UTT AMIS wamekuwa na ukuaji wa zaidi ya asilimia 12 ambao kwa utendaji wa soko la fedha kwa sasa faida hiyo ni nzuri.
“Utendaji wa soko la fedha kwa sasa faida hiyo ni nzuri sana, mwekezaji mkubwa ambaye ana pesa nyingi na mwekezaji mdogo ambaye ana pesa kidogo wote wanapata asilimia ile ile na ndiyo maana ya uwezeshaji wa mifuko hii,” alisema.
“Tumejitahidi sana kuwafikia wananchi wengi wadogo wadogo na sasa hivi tunaona vijana wengi wanajiunga na mifuko hii.”
Migangala alisema hadi sasa muitikio wa wawekezaji wengine wa kawaida ni mkubwa hali inayopelekea kuongezeka kwa umakini kwenye masoko ya fedha.
Naye Mkurugenzi wa Masoko UTT Amis, Daud Mbaga amesema mfuko umeendele kuboresha njia zake za uwekeza ambapo awali ilimbidi mwekezaji wa UTT AMIS aende benki moja kwa moja ili kununua vipande, lakini kwasasa Mwekezaji anaweza kununua vipande kupitia njia zote za malipo za benki ya CRDB yaani Simbanking, CRDB App na Fahari Huduma.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia