November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Gwajima azindua mradi wa kanzi data ya maarifa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka Taasisi ya Mashirikia Yasiyo ya Kiserikali TANGO kusaidia wanachama wake katika maeneo ambayo yanawakwamisha kuendesha shughuli zao vizuri hasa matumizi ya takwimu.

Dkt. Gwajima amesema hivyo wakati akizindua mradi wa Kanzidata ya Maarifa kwa ajili ya Asasi za Kiraia jijini Dar es salaam Julai 31, 2023.

“TANGO inatakiwa kuwa na uwezo zaidi na kuendelea kuhakikisha wanachama na wadau wake wana uwezo wa kutumia mradi huo ili kuwasaidia katika takwimu na ripoti lakini pia kuchangia kwenys maendeleo ya Taifa”. amesema Gwajima na kuongeza

“Kwa utafiti uliofanywa chini ya mradi huu wa Data Driven Advocacy (DDA), inaonyesha kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wadau wa AZAKI kutumia takwimu wakati wa shughuli zao za uchechemuzi.” amesisitiza Dkt. Gwajima.

Amebainisha pia mradi huo wa Kanzidata ya Maarifa kwa ajili ya Asasi za Kiraia utakuwa ‘One-stop Centre’ ya maarifa kwa wadau wote wa Sekta ya AZAKI, ambapo zitaungana pamoja na Wadau wa Maendeleo ili kupeana uzoefu wa kazi zao hivyo mabadiliko Chanya ndani ya jamii yatakuwa endelevu.

Serikali itaendelea kushirikiana na TANGO kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na takwimu na taarifa ili kuhakikisha TANGO inaweza kutekeleza mradi huu kwa weledi wa kutosha.

Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima ameonesha kufurahishwa na mpango wa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo huo pamoja na mijadala itakayofanyika kutokana na taarifa zitakazowekwa kwenye kanzidata na Wadau, hali itakayohamasisha majadiliano chanya yanayoendeshwa na takwimu na taarifa zilizotengenezwa na Wadau wote wakiwemo AZAKI.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji TANGO, Mr. Adamson Nsimba amewaasa wadau mbalimbali kushirikiana katika suala la kanzidata ili kusaidia taasisi nyingine nyingi ambazo zinakosa taarifa kupata chanzo cha maamuzi

Naye Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Data Driven Advocacy (DDA), Tanzania, Wakili Daniel Lema amesema TANGO watafanya jukumu la kuhakikisha maudhui yatakayowekwa kwenye Kanzi data ni yale ambayo yamechambuliwa na yenye mantiki ambayo yanaakisi uhalisia wa maisha ya jamii zetu.

“Niwaombe wadau wote hasa wa maendeleo tuweze kuunga mkono juhudi ya TANGO katika kuboresha jukwaa hili ili tuweze kuhakikisha mashirika yaliyo pembezoni yanafikiwa na kuelimishwa na kuwezeshwa ili kujua namna ya kutumia jukwaa hili kwa manufaa yao” amesema Wakili Daniel Lema.