Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule amesema kuwa kuelekea sherehe za maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini ambayo hufanyika kila mwaka nchini kuanzia Agosti moja na kufikia kilele Agosti 8 kwa Kanda ya Kati imejipanga kuja na mbinu za kupambana na mabadiliko ya Tabianchi.
Senyamule amesema utafiti unaonesha Mkoa wa Dodoma na Singida imeendelea kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo mifugo na uvuvi,kutokana na hilo amesema Mikoa hiyo imedhamiria kusambaza mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa Mazingira.
Mkuu wa Mkoa huyo ameeleza jijini hapa leo,July 31, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu sherehe na maonyesho ya nane nane Kanda ya kati ambapo ametaja Mbinu hizo kuwa ni pamoja kuhifadhi maji na udogo mashambani zikijumuisha matumizi ya makingamaji, kilimo cha mbegu tisa na jembe la mzambia, kuzalisha mazao yanayotumia maji kwa ufanisi (Mtama na alizeti), uzalishaji wa malisho kwa ajili ya mifugo, hifadhi ya misitu na upandaji wa miti, matumizi ya nishati mbadala (Jua, umeme na gesi) kwa ajili ya kupikia.
“Tutajikita zaidi kusambaza teknolojia za kisasa katika kilimo na ufugaji bora ambapo Taasisi za utafiti za kilimo, mifugo na uvuvi zitashiriki maonesho hayo kuonesha teknolojia mbalimbali zilizozalishwa kwenye vituo vya utafiti na kuwawezesha wakulima kunufaika na elimu ya uzalishaji bora,”amesema Senyamule.
Aidha ameeleza namna maonesho hayo yatakavyo adhimishwa Kanda ya Kati ambapo amesema kutakuwa na matukio muhimu ya Maonyesho ya nane nane 2023 ikiwemo kongamano la Tasnia ya Alizeti, kongamano la zao la mtama, siku maalumu ya uhamasishaji uzalishaji kuku wa kienyeji pamoja na Tamasha la mashindano ya nyama choma.
Pia ametaja Kauli mbiu ya Maonesho na Sherehe za Nane Nane Kitaifa kwa mwaka 2023 ni kuwa ni “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula” huku Kaulimbiu ya Kikanda ikiwa ni “Kilimo ni Biashara, Biashara ni Uwekezaji”
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa