Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online
NOVEMBA 25 hadi Desemba 10 ya kila mwaka Mataifa yote ulimwenguni huadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Maadhimisho haya yalianzishwa rasmi mnamo mwaka 1991 ambapo mwaka huu wa 2023 yatatimiza miaka 32 yakiwa na lengo kuu la kupinga vitendo vya ukatili na kuweka mikakati mbalimbali ya jinsi ya kutetea haki za wanawake na watoto.
Tunapozungumzia vitendo vya ukatili, tunamaanisha ni kitendo chochote anachotendewa mtu kitakachomsababishia madhara ya kimwili, kiakili au kisaikolojia yaani ni vitendo vyenye kusudio la kulazimisha au kutisha mtu na kujikuta akifanya jambo kinyume na matakwa yake.
Kiuhalisia ukatili umegawanyika katika takriban makundi makuu manne hivi ikiwemo ukatili wa kimwili, kingono, kiuchumi na ule wa kisaikolojia au tunaweza kusema wa kihisia, mtu anapotendewa moja ya mambo hayo anakuwa ametendewa ukatili.
Pamoja na kampeni mbalimbali zinazoendelea kufanyika hapa nchini kwa lengo la kupiga vita vitendo vya ukatili, lakini bado kasi ya upunguaji wa vitendo hivyo ni ndogo kutokana na baadhi ya watu kuuona ukatili mwingine kama jambo la kawaida pale unapofanyika miongoni mwa jamii.
Baadhi ya vitendo vinavyoonekana kuwa ni vya kawaida ni ukatili wa Kisaikolojia ambao mtu hufanyiwa huku jamii ikiona ni kawaida mfano, kutukanwa, kufanyiwa dhihaka, kudhalilishwa, vitisho vya kuuawa, wivu wa kupindukia, kunyimwa mafunzo, Gubu na kupitia ujumbe mfupi (sms) kwenye simu unaomdhalilisha au kutisha mtu.
Jamii kuendekeza Mila na desturi kandamizi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuendelea kufanyika kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia miongoni mwa makabila hapa nchini mfano, mwanamke aliyefiwa na mumewe kulazimiswa kurithiwa na ndugu pasipo ridhaa yake.
Tabia hii ya kulazimishwa kurithiwa na ndugu wa mwanamume ni miongoni mwa mila za kiafrika ambazo baadhi ya makabila hapa nchini wanaziendeleza hali inayowaathiri kisaikolojia wanawake wengi na wakati mwingine hujikuta wakiambukizwa magonjwa bila ya wao kutarajia.
Vile Tanzania bado inakabiliwa na wimbi kubwa la ukatili dhidi ya watoto wa chini ya umri wa miaka 18 hasa watoto wa kike ambao miongoni mwao hufanyiwa ukatili wa kunyimwa elimu kwa lengo tu la wazazi wao kutaka waolewe ili wapate mali zinazotolewa kama mahari.
Mbali ya ndoa za utotoni lakini pia bado lipo wimbi kubwa la watoto kubakwa au kulawitiwa hasa wale wa kiume na kuwasababishia madhara makubwa ikiwemo kupata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ukosefu wa kinga mwilini (UKIMWI) na mimba katika umri mdogo.
Tukumbuke haki za watoto zinalindwa katika mikataba mikubwa miwili ya kimataifa, ambayo ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990, yote hii imeridhiwa pia na nchi yetu ya Tanzania.
Vilevile kwa hapa Tanzania tuna Sheria ya Haki za Mtoto ya mwaka 2009 ambayo inataja haki za msingi za mtoto kama zilivyoelezewa kwenye mikataba hiyo na kueleza wazi kwamba katika kufanya maamuzi yoyote kuhusu mtoto kanuni ya maslahi bora ya mtoto lazima izingatiwe.
Mikataba hii na Sheria ya mtoto inatoa wajibu kwa Serikali, wazazi, walezi na wanajamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na ubaguzi ili kuhifadhi ustawi na makuzi yao.
Mfano katika mwaka 2021, masuala makuu yaliyoathiri haki za watoto kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi ni pamoja na ukatili wa kingono, ukatili wa kimwili na kisakolojia, ajira kwa watoto na utumikishwaji wa watoto, usafirishaji haramu wa watoto, ndoa za utotoni, na mimba za utotoni.
Takwimu hizo za polisi zilionesha matukio ya ukatili dhidi ya watoto yalipungua kutoka matukio 15,870 mwaka 2020 hadi matukio 11,499 kwa mwaka 2021, sawa na punguzo la asilimia 27.5 lakini bado asilimia 85 ya waathirika wa matukio hayo 11,499 walikuwa ni watoto wa kike, huku asilimia 15 iliyobaki ikiwa ni watoto wa kiume.
Vilevile takwimu ambazo zimewahi kutolewa na Shirika la Nukta Tanzania zinaonesha asilimia 22.8 ya wanawake hapa nchini waliolewa wakiwa hawajafikisha umri wa miaka 18 huku asilimia 37.2 ya wanawake walioolewa chini ya umri huo hawakuwahi kupata elimu rasmi.
Changamoto ya watoto wa kike kukatishwa masomo yao bado ni kubwa katika maeneo mengi hapa nchini hali ambayo inaonesha kuhitajika zaidi kwa nguvu za makusudi kukabiliana na sababu zinazosababisha watoto hawa wakatishe masomo yao ikiwemo ndoa katika umri mdogo.
Matukio ya hivi karibuni katika mikoa ya Shinyanga ambako mkuu wa mkoa huo alilazimika kuvunja ndoa ya mwanafunzi wa kidato cha tano iliyokuwa ikifungishwa katika kata ya Mwawaza na kule mkoani Ruvuma wazazi waliokuwa wakimuozesha mtoto wao kwa mahari ya shilingi 30,000 ni ushahidi tosha kwamba bado jamii haijakubali kubadilika.
Mkoani Shinyanga takwimu kutoka Ofisi ya elimu ya mkoa zinaonesha kwamba ndani ya kipindi cha mwaka mmoja pekee wa 2021/2022 watoto wa kike wapatao 1,358 waliacha shule kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba na ndoa za utotoni.
Ofisa elimu wa mkoa wa Shinyanga, Dafroza Ndalichako anasema katika kukabiliana na changamoto ya utoro wa wanafunzi hasa wale wa kike na umbali wa shule za sekondari za kata hivi sasa mkoa huo umejiwekea mikakati kadhaa ili kukabiliana na changamoto hizo.
Ndalichako anasema mkoa wa Shinyanga una shule za sekondari za kata 22 zenye hosteli kwa ajili ya wanafunzi na nyingine 10 kwa upande wa sekondari za Serikali Kuu na kwamba tayari kiasi cha shilingi 3,623,343,372.00 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya sita za sekondari.
“Mikakati tuliyonayo hivi sasa katika kukabiliana na changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kutoka kijijini kwenda shuleni ni kujenga sekondari mpya za kata ambazo hazina shule hadi sasa, na shule moja ya bweni kwa ajili ya watoto wa kike kupitia mradi wa SEQUIP,”
“Awamu ya kwanza zimejengwa shule sita kwa gharama ya shilingi 6,920,000,000.00 na tayari wanafunzi wanasoma ambapo shule sita nyingine zinatarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni ikiwa ni awamu ya pili kwa gharama ya shilingi 3,623,343,372.00,” ameeleza Ndalichako.
Katika kukabiliana na vitendo hivi vya ukatili hapa nchini waandishi wa habari kutoka mikoa 10 ya Tanzania wameanzisha Mtandao wa Kupiga Vita na Kupambana na vitendo vya Ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini unaofahamika kwa jina la Tanzania Journalist Against Violence & Gender (TAJOGEV).
Malengo makuu ya mtandao huu ni kutaka kuhakikisha jamii hapa nchini inabadilika na kuwachana na mila na desturi kandamizi na zilizopitwa na wakati na iwe na elimu ya kutosha kuhusu madhara makubwa yanayompata mtu anapotendewa kitendo chochote cha ukatili hasa upande wa wanawake na watoto.
Mwenyekiti wa TAJOGEV, Stella Ibengwe anasema waandishi wa habari ambao ni wanachama wa mtandao huo wanaamini iwapo wataungana pamoja katika kupaza sauti kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia kuna uwezekano mkubwa wa vitendo hivyo kupungua kama siyo kumalizika kabisa hapa nchini.
Mratibu wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mkoani Shinyanga, Glory Mbia mbali ya kuwapongeza waandishi kwa hatua waliyochukua ya kuanzisha mtandao wa kupiga vita vitendo vya ukatili anawataka wanahabari kuhakikisha wanaandika habari zitakazoleta mabadiliko makubwa katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini.
“Niwapongeze sana kwa hatua yenu ya kuanzisha mtandao huu wa TAJOGEV, ni jambo jema sana, naamini kupitia kalamu zenu mtawezesha kusambaza maeneo mengi elimu kwa jamii ya kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini, cha kuwaahidi ni ushirikiano wetu pindi mkiuhitaji,” anaeleza Mbia.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi amesema maeneo mengi hapa nchini bado yanakabiliwa na vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto na kwamba kupitia Mtandao wa TAJOGEV anaamini vitendo hivyo vinaweza kupungua kama siyo kumalizika kabisa.
“Niwashukuru kwa kuliona hili tatizo na mkaamua kuanzisha mtandao huu, ni jambo jema, kikubwa ninachowaomba wakati mkipiga vita ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini pia tupieni macho upande wa wanaume, pia wapo wanaofanyiwa ukatili na wenza wao,”
“Wapo wanaume wanaokutana na matatizo mengi, wanafanyiwa ukatili lakini wanavumilia wakiona ni aibu iwapo watatoa taarifa za ukatili wanaotendewa majumbani na mara nyingi wengi wao hujikuta wakiathirika kisaikolojia, sasa pazeni sauti pia ili waweze kutoa taarifa juu ya ukatili uliopo ndani ya familia zao,” anaeleza Samizi.
John Myola ni Mkurugenzi wa Shirika la Agape la mkoani Shinyanga linaloshughulika na utetezi wa Haki za wanawake na watoto anasema hali ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika mkoa wa Shinyanga bado ipo hasa kwa upande wa watoto wa kike.
Myola ambaye kituo chake kinachowaendeleza kielimu waathirika wa mimba na ndoa za utotoni chenye watoto wa kike wapatao 57 anasema changamoto ya mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga bado inahitajika juhudi za makusudi katika kukabiliana nayo huku akiiomba Serikali pia kuweka mkono wake badala ya maneno matupu.
Anasema panahitajika juhudi kubwa ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kwamba Serikali kwa sasa iangalie uwezekano wa kuzipatia ruzuku asasi zisizokuwa za kiserikali (NGO’s) zinazojishughulisha na upigaji vita vitendo vya ukatili hapa nchini.
“Imefika wakati Serikali ioneshe kwa vitendo katika vita hii, maana mara nyingi wao wamekuwa wasemaji na wakemeaji tu lakini hakuna hatua za makusudi wanazochukua, sasa ioneshe kwa vitendo ushiriki wake katika vita hii, hasa kwa kutenga fungu la fedha kuzisaidia NGO’s zinazojishughulisha kupinga vitendo hivi vya ukatili,”
“Pili jamii iendelee kupatiwa elimu kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto hii itasaidia katika kupunguza kama siyo kukomesha kabisa vitendo hivyo hapa nchini, tukishikamana kwa dhati vitendo vya ukatili itabaki kuwa historia katika nchi yetu,” anaeleza Myola.
Kuhusu sheria zilizopo Myola anaishauri Serikali iangalie upya Sheria za makosa ya Jinai na Kanuni za adhabu zilizopo ili kuzifanyia marekebisho kuwezesha watuhumiwa wa makosa ya ubakaji wasiwe wanapewa dhamana ili kuzuia wasitoroke au kuharibu ushahidi mpaka pale watakapokuwa wamefikishwa mahakamani na kesi zao kusikilizwa na kutolewa hukumu.
Pia Serikali iendelee kuweka msukumo katika kuielimisha Jamii juu ya madhara yanayowapata watendewa wa vitendo vya ukatili ili ielewe na ichukue hatua za makusudi katika kuvipiga vita, maana pamoja na kila mwaka kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kasi ya kupungua kwa vitendo hivyo hapa nchini bado ni ndogo.
Wakati tukielekea kwenye maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili kwa mwaka huu ni jukumu letu sote kuangalia jinsi gani tutakuwa miongoni mwa askari shupavu wa kupambana na vita hii ambayo bado ni mbichi kutokana na kuendelea kutokea kwa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo ulawiti kwa watoto wa kiume.
More Stories
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta