November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPDC kuanza ukarabati kisima cha Mnazi bay Mtwara

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam.

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC limebainisha kuanza kwa zoezi la ukarabati wa kisima cha gesi asilia kilichopo Mnazi Bay Mkoani Mtwara hivi karibuni.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Uendelezaji na Uzalishaji wa Gesi TPDC, Eng. Felix Nanguka, amesema zoezi hilo la ukarabati wa Visima, hufanyika kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu litafanyika hivi karibuni katika kisima namba Moja kilichopo Mnazi bay.

” Katika kutekeleza majukumu ya msingi ya TPDC ambayo yameahinishwa na TPDC kisheria ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika inayotokana na gesi..hivyo TPDC inahakikisha gesi inapatikana kwa ajili ya upatikanaji wa umeme nchi nzima, hivyo tutakuwa na zoezi la ukarabati wa kisima cha Mnaz Bay kilichopo Mkoani Mtwara”, amesema Nanguka.

Nanguka amesema, nchi inategemea zaidi gesi asilia kwa asilimia 65 ili kupata umeme, hivyo kudai kuwa Shirika hilo linaowajibu wa kuhakikisha gesi inapatikana wakati wote.

” Uzalishaji umeme unategemea zaidi ya asilimia 65 kutoka katika gesi…hivyo sisi kama TPDC tunahakikisha gesi inapatikana wakati wote”, amesema Nanguka.

Aidha Nanguka ameongeza kuwa, zoezi hilo la ukarabati wa kisima utaambatana na ongezeko la uzalishaji katika kisima namba moja, kinachojulikana kama (MB ONE) kinachotoa umeme katika mikoa ya kusini Mtwara na Lindi na gesi nyingine kupelekwa katika Bomba kubwa kwa ajili ya matumizi mengine.

Pia ameongeza kuwa, kisima hicho huzalisha futi za ujazo takribani mil 11 kwa siku, ambapo baada ya zoezi Hilo kukamilika inatarajiwa kuwepo kwa ongezeko la gesi takribani futi Mil.7 kwa siku ambayo ni sawa na asilimia 65.