Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali ya Tanzania imepongezwa kwa kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Afya pamoja na kutoa ushirikiano kwa mashirika ya kimataifa hususan Shirika la Afya Duniani (WHO).
Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses wakati wa kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 28 julai 2023.
“Ninaipongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wenu ambao mmekuwa mkiutoa kwa Shirika la Afya Duniani, hakika tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano katika kuhakikisha kuwa tunaboresha na kuimarisha misingi ya sekta ya afya hapa Tanzania,” amesema Dkt. Sagoe-Moses.
Dkt. Sagoe-Moses ameongeza kuwa juhudi za Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na magonjwa ya mbalimbali hususan yale ya mlipuko ni nzuri na zinaridhisha, mfano mzuri ni jinsi Tanzania ilivyopambana na homa ya Marburg katika mkoa wa Kagera.
“WHO tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukinga na kutibu magonjwa mbalimbali ili kuhakikisha kuwa afya za watanzania zinakuwa bora wakati wote,” aliongeza Dkt. Sagoe-Moses.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amemhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Dkt. Tax amesema kuwa Tanzania itaendelea kufanya kazi na WHO ili kuhakikisha kuwa inaboresha na kuimarisha mifumo ya afya na Sekta ya afya kwa ujumla pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa sekta ya afya ili kuwawezesha kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali yanayoibuka katika jamii.
“Tanzania na Shirika la Afya Duniani zimekuwa zikishirikiana katika kuimarisha na kuboresha sekta ya afya nchini, mchango wa WHO ni mkubwa na umeisadia Serikali kuboresha sekta ya afya na utekelezaji wa afua mbalimbali za mapambano dhidi ya magonjwa…..mfano mzuri tumekuwa tukishirikiana katika kutokomeza Malaria, Uviko 19 na magonjwa mengine kama vile HIV, ” alisema Dkt. Tax.
Tanzania imekuwa ikishirikiana na WHO pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha kuwa inaboresha mifumo ya afya na Sekta ya afya ili kuijengea uwezo nchi na wataalam wake katika kutambua na kudhibiti magonjwa.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa