November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Jackline agawa vitendea kazi kwa akina mama wauza kokoto

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MBUNGE wa viti maalumu kupitia UWT Mkoani Tabora Jackline Kainja amesaidia kikundi cha wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata ya Mpera, manispaa ya Tabora vitendea kazi vyenye thamani ya sh mil 1.5 ili kuboresha mradi wao wa kuponda na kuuza kokoto.

Vitendea kazi vilivyokabidhiwa na Mheshimiwa Mbunge kwa kikundi hicho cha wana UWT ni makoti 20, kofia ngumu 20, miwani 20, glovusi 40 na fedha taslimu sh 200,000.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika kata hiyo baada ya kukabidhi vifaa hivyo amepongeza kikundi hicho kwa jitihada zao nzuri za kujiongezea kipato kupitia mradi huo ndio maana akaguswa kuja kuwatembelea ili kuwaongezea ari ya kufanya vizuri zaidi.

Amebainisha kuwa vifaa alivyowapatia vitawarahisishia kazi na kuwaongezea uzalishaji ili kuongeza kipato zaidi na kuwawezesha kupiga hatua kubwa zaidi mbele.

Aidha amempogeza Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwaletea maendeleo watanzania pasipo kujali itikadi za vyama vyao.

Amewataka akinamama wote wa CCM na vyama rafiki kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais na kumsemea vizuri kwa wananchi ili aendelee kuwaletea maendeleo.

Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ramadhan Shaban Kapela ameahidi kuwainua zaidi akinanama hao kupitia dirisha la mikopo punde tu serikali itakapoweka utaratibu mwingine wa utoaji mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu kupitia asilimia 10 za mapato ya halmashauri.

Katika mkutano huo makada wa CCM Shaban Mrutu (Mkurugenzi wa Chuo cha Tabora Polytechnique), Grace Kape na diwani wa viti maalumu waliunga mkono juhudi za Mbunge Jackline kwa kukiongezea mtaji wa sh laki 5 kikundi hicho cha wanawake wauza kokoto.

Mbunge wa viti maalumu CCM kupitia Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoani Tabora Jackline Kainja (aliyevaa gauni la kijani mbele) akifurahia na kikundi cha akinamama wauza kokoto wa UWT kata ya Mpera katika halmashauri ya manispaa ta Tabora baada ya kuwamwagia vitendea kazi ili kuwarahisishia kazi ya upondaji na uuzaji kokoto hapo jana. Picha na Allan Vicent.