November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar yazinduliwa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kupitia Idara ya Msaada wa Kisheria Zanzibar kwa kushirikiana na Legal Services Facility (LSF) wamezindua maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar kwa mwaka 2023 kwa ajili ya kutoa elimu pamoja na huduma za msaada wa kisheria katika jamii ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji wa huduma hiyo.

Maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar yanafanyika huku yakipambwa na shughuli mbalimbali za kijamii lengo likiwa na kuhamasisha jamii kufikiwa na huduma za msaada wa kisheria popote zilizo bila kikwazo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo Zanzibar, Waziri Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema kuwa maadhimisho hayo yanakuja ikiwa ni hatua ya serikali kuwajali wananchi wake.

“Shughuli ni muhimu kwakuwa tunalenga kuhakikisha kuwa Zanzibar inazungukwa na jamii yenye ustawi mzuri uliomarika katika kila nyanja ya maisha pamoja na kuhakikisha wananchi wake hususani wanyonge na wasiojiweza wanapatiwa msaada wa kisheria bila ya usumbufu wowote. Lengo kuu la Wiki ya Msaada wa Kisheria ni kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa jamii yetu inayotuzunguka.” amesema Waziri Suleiman.

Kwa upande wake, Afisa Programu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Legal Services Facility Visiwani Zanzibar, Alphonce Gura amesema kuwa LSF ni mdau mkuu katika maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar kwakuwa tukio hilo linalenga kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi ili kuongeza upatikanaji wa haki pasina kikwazo chochote kile.

“LSF kazi yetu kubwa ni kukuza upatikanaji wa haki kupitia uwezeshaji wa kisheria kwa wananchi wote hususani wanawake na wasichana. Hivyo kupitia maadhimisho haya tutaweza kuwafikia watu wote kupitia shughuli mbalimbali ambazo zinakwenda kufanyika katika kipindi hiki cha maadhimisho,” amesema Gura.

Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika katika wiki hiyo ni pamoja na utoaji wa elimu ya kisheria kupitia vyombo vya habari, uendeshaji wa jukwaa la kona ya msaada wa kisheria ili kuyafikia makundi yote katika jamii, kutembelea makundi yaliyoko vizuizini (magerezani/rumande au vyuo vya mfunzo) pamoja uandaaji wa bonanza la msaada wa kisheria kwaajili ya kupaza sauti kuhusu kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji katika jamii.

Maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar 2023 ambayo yamezinduliwa tarehe 15 Julai 2023 yatarajiwa kutamatika rasmi mnamo tarehe 22 Julai 2023 visiwani Zanzibar, ambapo Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ndio atakuwa mgeni rasmi wakati sherehe za kilele, ambazo zitafanyika sambamba na utoaji tuzo kwa wasaidizi wa kisheria visiwani humo.

Waziri Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar mwaka 2023.
Afisa Programu Mwandamizi kutoka Ofisi za Legal Services Facility (LSF) Visiwani Zanzibar, Alphonce Gura akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar mwaka 2023.