November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCRA kuja na bendi za masafa zitakazotumiwa bure na watoa huduma

Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)imesema
ipo katika hatua za awali za kufungua bendi za masafa ambazo zitatumiwa na watoa huduma bure bila kuhitaji kuwa na leseni ya rasilimali masafa,hatua ambayo itaongeza matumizi ya Intaneti kwa kuwa na huduma za intaneti za wazi (WiFi -hotspots).

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Julai 18 ,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt.Jabir Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa mwaka 2023/24.

Dkt.Jabir amesema kuwa hadi sasa
TCRA imefanikiwa kugawa masafa yanayowezesha utoaji wa huduma ya intaneti ya kasi kwani malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2025 asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma ya intaneti ya kasi.

Wakati huo huo amesema kuwa tozo ya miamala ya fedha kupitia simu za mkononi imepungua kutoka 19,225,082,685 mwezi Julai, 2022 hadi kufikia 14,805,512,341 mwezi Juni, 2023 ambayo ni sawa na 22.99%.

Amesema kupungua kwa tozo ya miamala ya fedha imesababishwa na kupungua kwa viwango vya tozo ya miamala ya fedha vilivyoanza kutumika tarehe 1 Oktoba, 2022.

Pia ameeleza kuwa mwenendo wa gharama za rejareja za kupiga simu kwa kutumia kifurushi ndani na nje ya mtandao kuanzia 2015 hadi sasa, zimeendelea kushuka na kuwezesha watu wengi waweze kumudu gharama hizo.

“Julai, 2022 bei ya dakika ndani ya mtandao kwenye kifurushi (Tsh/Dakika) ilikuwa ni 7.7. Hadi kufikia Juni, 2023 bei imepungua kufika 5.19,”amesema.

Aidha ameeleza Uwiano baina ya mitandao na matumizi unaonyesha kuwa maeneo mengi yamefikiwa na huduma za Intaneti ila watumiaji ni wachache, sababu ikiendelea kuwa ni idadi ndogo ya watumiaji wenye simu janja, hivyo kupelekea kuwepo na umuhimu wa TCRA kufuatilia kwa kina gharama za simu janja.

“Serikali imeridhia punguzo la ada za mwingiliano wa mawasiliano ya simu za Kimataifa kutoka Dola za Marekani senti 25/kwa dakika hadi kiwango cha Dola za Marekani senti 10/kwa dakika. Utaratibu huu umeanza kutumika mwezi Julai, 2023 na hatua hii itachochea ukuaji wa uchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,”amesema.

Hata hivyo amesema kuwa kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, hadi kufikia Juni 2023, Tanzania imeendelea kuwa nchi yenye kiwango kidogo sana cha bei ya data kwa GB 1 ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo gharama ya GB 1 ni Dola za Marekani 0.71 sawa na shilingi 1,666.

“Pia kwa kiwango hicho hicho, Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa bei ndogo ya data kwa GB 1 ukilinganisha na nchi zote zilizopo SADC na hii ni kwa mujibu wa ripoti ya “Worldwide Mobile Data Pricing 2022,

“Tanzania pia inashika nafasi ya saba kwa kuwa na bei ndogo ya data kwa Afrika, hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa katika tovuti statista,
ambapo katika Bara la Afrika, takwimu hizo zinaonyesha kuwa wastani wa gharama ya GB 1 ni Dola za Marekani 3.51 hii ni sawa na shilingi 8,157,”amesema.

Akizungumzia mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli zilizopangwa kwa mwaka amesema kuwa
TCRA itaendelea kusimamia usalama mtandaoni kupitia TZ-CERT kwa kufanya tathimini ya mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwa lengo la kubaini madhaifu ya kiusalama na kushauri juu ya hatua za kurekebisha na kujilinda na matishio ya usalama mtandaoni, itahamasisha uanzishaji wa Vikundi vya Kidijitali mashuleni na vyuoni kwa ajili ya kujenga uwezo wa TEHAMA kwa Wanafunzi, pia itasimamia uimarishaji na upatikanaji wa mawasiliano ya Redio nchi nzima.