November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walioshinda tuzo za EAC na SADC wameliheshimisha Taifa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Katibu Mkuu ,Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe ameonyesha kufurahishwa na vijana wa kitanzania walioshinda tuzo za uandishi wa insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) huku akisema wameliheshimIsha Taifa na Elimu ya Tanzania kwa ujumla licha ya changamoto za elimu zilizopo hapa nchini.

 “Vijana wamedhihirisa kuwa pamoja na changamoto zilizopo katika elimu yetu lakini bado inaweza kuhimili  kitaifa na kimataifa.”alisema Profesa Mdoe

Aidha amewataka walimu nchini kutokuwa changamoto ya kuwafanya wanafunzi washindwa kushiriki mashindano ya uandishi wa Insha na badala yake wawahamasishe na kuwapa miongozo ya kushiriki katika mashindano hayo.

Profesa Mdoe ameyasema hayo jijini hapa wakati wa hafla ya utoaji tuzo za uandishi wa Insha za EAC na  SADC 2021 kwa wanafunzi walioshinda huku akisema,mashindano hayo yanawajengea ujasiri zaidi wa kufanya vizuri hata katika masomo yao.

Amesema,hakuna haja ya kuwa sababu yoyote ya kuwafanya wanafunzi washindwe kushiriki mashindano huku akiwahimiza wazazi na walimu kuwa chachu ya wanafunzi wengi zaidi kushiriki katika mashindano hayo.

“Wanafunzi walioshiriki bado ni wachache ,sote kwa pamoja tudhamirie kuwahamasisha ili wanafunzi wengi zaidi waweze kushiriki mashindano hayo kila yanapotangazwa.”amesema Profesa Mdoe

Amesema,zipo taarifa kwamba kuna baadhi ya walimu ambao wamekuwa wakidhani mwanafunzi akishiriki kwenye mashindano hayo inaweza kumsababisha ashindwe kufanya vizuri kwenye masomo yake jambo ambalo amesema siyo sahihi.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo,mashindano hayo kwa wanafunzi ni kuwaongezea uwezo katika kukuza ujuzi wa lugha,unawaongezea maarifa kwa ujumla kwa kuwa na uelewa zaidi wa mambo mbalimbali.

“Mashindano haya pia yana umuhimu mkubwa kwa wanafunzi hawa,yanawapa hata fursa katika  kutumia muda mwingi katika mambo muhimu na kuwajengea ujuzi zaidi na kuwa mahiri zaidi katika masomo yao.”amesisitiza Profesa Mdoe

 Mratibu wa Insha kutoka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Matuha Masati alisema,mashindano hayo yamekuwa chachu kwa vijana hao kufanya utafiti,kujifunza na kupanua wigo wao wa kujifunza zaidi.

Kwa mujibu wa Matuha katika mashindano hayo jumla ya wanafunzi 133 walishiriki katika shindano la uandishi wa Insha za SADC kwa Mwaka 2021 ambapo washindi 10 walipatikana kwa ngazi ya Taifa lakini pia kwa upande wa wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ,wanafunzi 315 walishiriki katika mashindano hayo ambapo pia walipatikana washindi 10 na wote kwa pamoja walipewa zawadi mbalimbali zikiwemo Tuzo.