November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge ataka wanaopinga ubinafsishaji wa Bandari wapuuzwe

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Nkasi

MBUNGE wa viti maalumu mkoa wa Rukwa Bupe Mwakang’ata  (CCM) amewaondoa hofu Wananchi juu ya uwekezeji bandarini unaofanywa na serikali na kuwapuuza wale wote wanaoukashifu uwekezaji huo kupitia DP WORD

Akizungumza kwenye kikao cha  baraza la Wanawake UWT wilayani Nkasi amesema kuwa kumekuwepo na maneno mengi ya upotoshaji juu ya uwekezaji unaofanywa na serikali katika kuboresha shughuli za bandari Nchini na kuwa lengo ni kutaka kukuza mapato yatokanayo na bandari ili kipato kinachopatikana kiweze kutoa huduma kwa jamii.

Amesema ni muda mrefu serikali imekua ikitafuta namna nzuri ya kuleta tija katika bandari zetu Nchini na moja ya njia hizo ni za uwekezaji na sasa wamejitokeza watu ambao wanaupinga bila sababu za msingi na kutaka waende wakawe mabalozi wazuri na kuelezea nia njema ya serikali juu ya uwekezaji ambapo sasa DP WORD wameonyesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo la bandari.

“Uwekezaji katika eneo hili la bandari ni utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kukuza pato la taifa sasa wamejitokeza watu ambao ni wapotoshaji juu ya uwekezaji huo wa bandari na sisi tukawe chachu ya kulisemea jambo hili na kuuelimisha Umma juu ya umuhimu wa uwekezaji huo na tuwakemee wapotoshaji hadharani”alisema Bupe.

Na amedai kuwa bandari ina changia sehemu kubwa ya pato la taifa hivyo eneo hilo linahitaji maboresho ili tija zaidi ionekane na mojawapo ya kinachofanyika ni uwekezaji na Watanzania watambue nia njema ya serikali katika uwekezaji huo.

Sambamba na hilo mbunge huyo katika kuunga mkono jitihada za Mama Samia Suluhu Hassan za kukabiliana na uharibifu wa mazingira amewakabidhi Wanawake hao kila mmoja jiko la kupikia la Gesi ili kupunguza matumizi ya kuni yanayopelekea misitu kukatwa na kupata kuni.

Amesema kuwa njia sahihi ya kukabiliana na ukataji wa miti kiholela ni kuwa na matumizi ya nishati mbadala ikiwemo gesi na kutaka majiko hayo yatumike ipasavyo ili kuachana na matumizi ya kuni.

Aliwataka Wanawake hao wakawe chachu katika jamii wanayotoka juu ya matumizi ya njia mbadala ya nishati kwa kutumia gesi ili matumizi ya kuni yapungue kwa kiasi kikubwa katika jitihada za kulinda mazingira kunakotokana na shughuli za kila siku hasa kupata nishati ya kupikia.

Mwenyekiti wa UWT wilaya Nkasi Beatrice Ngua kwa upande wake alimshukuru Mhe,Mbunge kwa kujitoa na kuwakabidhi mitungi hiyo ya gesi zaidi ya 70 na kuwa wao watayatumia vyema ikiwa ni pamoja na wao kwenda kuwa chachu kwa Wanawake wenzao juu ya matumizi ya nishati mbadala badala ya kutegemea kuni pekee ili kuweza kuyalinda mazingira.

Na alidai kuwa wao watajitahidi kuuelimisha Umma juu ya nia njema ya serikali ya kuboresha utendaji wa bandari Nchini na uwekezaji katika eneo hilo haukwepeki na kumtaka kila mmoja akawe mstari wa mbele kulisemea hilo ili jamii iweze kuelewa na kuwapinga wapotoshaji wote.

Mbunge wa viti Maalumu mkoani Rukwa Bupe Mwakang`ata akikabidhi majiko ya gesi kwa Wanawake wa UWT wilayani Nkasi kama njia ya kuiunga mkono serikali kukabiliana na uharibifu wa mazingira