Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma
MKUU wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema,watoto wanapaswa kulelewa kwa kupatiwa mahitaji yao ya msingi ili waweze kukua vyema.
Brigedia Jenerali Mabena ameyasema hayo wakati JKT ikikabidhi msaada wa chakula na mahitaji mengine kwa watoto wanaoishi katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo jijini Dodoma huku akisema,ni vizuri watoto wakalelewa kwa kufuata misingi yote ya malezi na makuzi yao ili Taifa liweze kupata nguvukazi ya kutosha na yenye tija hapo baadaye.
“Kituo hiki kina watoto wa darasa la elimu ya awali,kina eneo la kufugia samaki na shughuli nyingine,lakini JKT linafanya kazi ya malezi ya vijana ,uzalishaji mali na ulinzi wa Taifa ,kwa hiyo vijana tunaowalea nao walikuwa wadogo kama hawa,kwa hiyo tutashirikiana na kituo hiki katika shughuli za uzalishaji hasa shambani na kwenye ufugaji wa samaki ,”amesema Brigedia Jenerali Mabena na kuongeza kuwa
“Vijana wetu wanafanya shughuli mbalimbali zikiwemo uzalishaji mali hasa katika kilimo na ufugaji ,kwa hiyo tunapovuna wanakula vijana wenyewe ,lakini safari hii tukaona chakula hiki tushirikiane na watoto wa Kikombo katika kuadhimisha miaka 60 ya JKT.”
Aidha amesema,msaada wa chakula uliopelekwa na JKT katika Makao hayo ya Watoto ni mchele kilogramu 500 ,unga wa ugali kilogramu 500 ,maharagwe kilogramu 200,sukari kilogramu 50,mafuta ya kupikia lita 60,juisi katoni 14,mbuzi wawili na chumvi katoni mbili.
“Lakini tutaendelea kushirikiana na Kituo Hiki katika malezi ya Vijana kuweza kuwapa Maarifa hasa katika shughuli za mbalimbali za uzalishaji ukiwemo ufugaji wa samaki kwaajili ya kupata lishe bora kwa watoto itakayowasaidia kukua vyema na kuleta tija katika Taifa.
Kamishina Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Makundi Maalum Tullo Masanja amesema,Nyumba ya Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo inahudumia watoto 131 ambapo hupokea watoto wa umri wa kuanzia miaka miwili hadi 17.
Aidha amesema msaada huo ulioletwa na JKT una manufaa makubwa hasa kwa ajili ya kuboresha lishe ya watoto ambayo ina mchango mkubwa katika suala zima la malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
“Hili ni kundi ambalo bado linahitaji msaada kutoka kwa jamii ,na moja ya kitu muhimu kwa binadamu ni chakula ,mtoto anapopata chakula na kupata lishe sahihi inamsaidia hata kukua kwa akili yake,inaongeza furaha na uchangamfu katika maisha yake,kwa hiyo ni jambo kubwa sana kwa vitu vilivyoletwa vina mchango mkubwa katika mchangokatika makuzi ya kiakili ,ya kiafya kwa watoto.”amesema Tullo
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha kulelea watoto Kikombo, Johnas Tarimo ameshukuru na kupongeza jitihada za Jeshi la Kujenga Taifa kusaidiana na Wizara katika kutoa stadi za kazi kwa watoto waliopo kwenye Makazi hayo kwani itakua chachu kwa watoto hao kujifunza zaidi kwa vitendo.
“Watoto hujifunza zaidi kwa kuona ,kwa hiyo hata uwepo wenu leo hii ni motisha tosha ya wao kushawishika kuwa kwenye kundi la vijana wenye manufaa na tija kwa Taifa hapo baadae ,
“Lakini pia huenda wapo baadhi yao wameshavutiwa nanyi na pengine wanaweza kutamani kuwa walinzi wa Taifa siku moja” amesema Tarimo
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa