Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Mwanza
Masha Mshomba Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), amebainisha mbele ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, changamoto kubwa iliyopelekea kuchelewa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano iliyopo jijini Mwanza eneo la Capripoint inayomilikiwa na NSSF ni kutokuwepo kwa muendeshaji hoteli wa kimataifa.
Mshomba amesema hayo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyetembelea mradi huo tarehe 14 Juni, 2023. Hata hivyo amebainisha kuwa kuanzia mwezi Juni mwaka 2024 hoteli hiyo inatarajiwa kukamilika na kuanza kazi rasmi.
Alisema katika uzoefu walioupata kwa wenzao wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya nchi Jirani ikiwemo Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe ni kwamba huwezi kumalizia hoteli ya nyota tano kabla hujapata muendeshaji wa hoteli.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia vile hatukupata muendeshaji wa hoteli kipindi kile ndio maana mradi ulishindikana kukamilika,” alisema Mshomba.
Alisema ilipofika mwaka 2017/18, Mfuko ulitangaza zabuni ya muendesha hoteli hata hivyo hakupatikana kutokana na mazingira ya kipindi hicho na mwaka 2019 mwezi Septemba walienda nchini Zambia na Afrika Kusini ili kupata uzoefu jinsi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya nchi hizo inavyopata waendeshaji wa hoteli ambapo NSSF ilipata kampuni ya Hilton Hotels Worldwide, Radissons Hotels na Legacy Hotel.
Mshomba alisema ilipofika mwezi Machi 2021, shughuli za ujenzi ziliendelea na walianza kumtafuta msanifu wa kuandaa michoro na mahitaji muhimu kwa ajili ya kumalizia kazi za ndani kwa viwango vya kimataifa (interior designer Architect) M/s SOURCE IBA toka Afrika Kusini.
Alisema mwezi Septemba 2022 walitangaza zabuni ya kumpata muendesha hoteli wa kimataifa, na kwamba kipindi hicho zile kazi ambazo zinahitajiwa kuendelea kabla ya kuwa na muendesha hoteli zilikuwa zinaendelea kama vile ujenzi wa vyoo na madirisha.
Mshomba alisema mpaka sasa baada ya kutangaza zabuni wamewapata waendesha hoteli watatu ambao waliomba zabuni ikiwemo kampuni ya Hilton Hotels Worldwide, Radissons Hotels na Legacy Hotel, ambapo mwishoni mwa mwezi huu wanatarajia kupata mshindi.
Alisema baada ya kupatikana kwa muendesha hoteli, wanatarajia hadi kufika mwezi Juni 2014 ujenzi wa hoteli hiyo uwe umekamilika na kwamba itachangia sana shughuli za kitalii jijini Mwanza.
Aidha, ameomba kukamilika kwa mradi wa hoteli hiyo kuende sambamba na kuendeleza uwanja wa ndege wa Mwanza.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni vema jambo hili likaenda sambamba na kuendeleza uwanja wa ndege wa Mwanza maana yake watu watakapokuja kutalii watahitaji kulala katika hoteli hii ya nyota tano,” alisema Mshomba.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania