December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB yatakiwa kutoa mikopo kwa wakulima, kuchochea uchumi

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa

BENKI ya CRDB imetakiwa kuendelea kutoa mikopo kwa Wakulima kwani kufanya hivyo kutachochea kwa haraka kupanda kwa uchumi hasa kwa wakulima wadogo ambao wataongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Wito huo umetolewa jana na mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali kwenye ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya CRDB wilayani Nkasi ambapo amedai kuwa mikopo zaidi kwa Wakulima inahitajika na ipo haja kwa benki hiyo kuendelea kutoa mikopo mingi kwa wakulima hasa wadogo wadogo.

Amesema kuwa kasi iliyopo sasa ya kufungua matawi ya benki katika maeneo mbalimbali kunawafanya wao kuwa karibu zaidi na Wananchi hivyo ni muhimu sasa kwa benki hiyo kutengeneza mazingira ya uwezeshaji kwa Wananchi kwa kuwapatia mikopo mbalimbali.

Mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa fedha ni kichocheo muhimu katika ukuzaji wa uchumi hivyo benki hiyo pia iwe na jukumu la kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya rasilimali fedha ili kila mmoja aweze kujua matumizi sahihi ya rasilimali hiyo katika kuweza kujikwamua kiuchumi .

Pia aliipongeza benki ya CRDB kwa kuwa na ubunifu mkubwa wa mifumo mbalimbali ya kurahisisha huduma za kibenki na Wananchi kuendelea kupata huduma hizo kwa wakati na kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi.

Na alifafanua kuwa benki hiyo wana kauli mbiu ya “ulipo tupo” kuwa ikienda kwa vitendo benki hiyo itachagiza kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa hili.

Awali kaimu mkurugenzi wa wateja wadogo toka makao makuu ya benki Yusto Ngwelo alidai kuwa benki hiyo sasa ina matawi 252 na mawakala kila eneo na lengo lao kuu ni kuwasogelea Wananchi pale walipo ili kila  mmoja aweze kupata huduma za kibenki popote pale alipo iwe mjini ama kijijini.

Amesema kuwa licha ya wao kutoa huduma za kifedha pia wamejikita kwenye utoaji wa huduma za bima tofauti ikiwemo za afya ili kila mmoja aweze kufikiwa na huduma hiyo muhimu.

Meneja wa kanda ya nyanda za juu kusini Jaffari Asanari kwa upande wake  aliwataka watu kuendelea kuzitumia huduma zao za kibenki kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kujikwamua kiuchumi na kuwa sasa wameanzisha kitu kinaitwa “IMBEJU” huu ni mpango maalumu kwa ajili ya mikopo ya Wanawake na vijana na akawaomba wautumie mpango kwani utawasaidia sana hasa Wanawake katika kujikwamua kiuchumi.

Hamisi Shabani ambaye ni mkazi wa mji wa Namanyere alidai kuwa uwepo wa benki hiyo kwao kutarahisisha sana kuweza kupata huduma za kibenki kiurahisi na wao kuweza kujiendeleza kiuchumi.

Meneja wa CRDB kanda ya nyanda za juu kusini Jaffari Asanari akitoa maelezo juu ya nini dhamira ya benki hiyo kuweka tawi jipya Kasi
Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali wa pili kutoka kushoto akikata utepe kuashiria ufunguzi wa benki tawi la Nkasi.