November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wauguzi wanaotuhumiwa kusababisha kifo cha mapacha wasimamishwa kazi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKUU wa Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Dkt Rashid Chuachua ameagiza kusimamishwa kazi Watumishi 2 wa Kituo cha Afya Kaliua wanaotuhumiwa kuzembea kumhudumia mama aliyejifungua mapacha 2 lakini wakapoteza maisha kwa kukosa huduma.

Akizungumza na gazeti hili DC Chuachua amesema kuwa amelazimika kuchukua hatua hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma wa sakata hilo lililopelekea kupoteza maisha watoto hao licha ya mama kujifungua salama.

Alisema baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baba mzazi wa watoto hao Issaka Raphael (30) Mkazi wa Ushokola wilayani humo, akilalamikiwa uzembe wa watoa huduma waliokuwepo zamu usiku huo, aliitisha kikao cha dharura cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambacho kiliazimia kusimamishwa waauguzi 2 ili kupisha uchunguzi.

Alibainisha kuwa wakati wakisubiri taarifa ya uchunguzi wa kifo hicho, miili ya watoto hao imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Urambo, wilayani Urambo kwa kuwa hospitali ya wilaya Kaliua haina jokofu la kuhifadhia maiti.

‘Naomba wazazi na jamii kwa ujumla waendelee kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi wakati wa zoezi la uchunguzi wa chanzo cha kifo kwa watoto hao’, alisema.

Awali baba mzazi wa watoto hao Issaka Raphael (30) alisema mke wake Mseneza Benson (25) alifikishwa katika Kituo cha Afya Kaliua Mei 9, 2023 majira ya saa 1 jioni baada ya kupata uchungu na kufanikiwa kujifungua salama majira ya saa 5 usiku.

Alisema baada ya kujifungua Muuguzi alimweleza kuwa watoto wako salama ila  walikuwa hawajafikisha muda wa kuzaliwa (njiti), hivyo wanatakiwa kupelekwa hospitali ya Misheni Kaliua ili kuwekwa kwenye chumba maalumu ambapo walitakiwa kutafuata usafiri wa kumpeleka mama na watoto.

Alisema aliatafuta usafiri hadi akaupataila alipowaeleza wauguzi kuwa tayari bajaji imefika aliambiwa asubiri wanawaandaa kitendo alichodai kilichukua muda wa zaidi ya masaa 2 pasipo sababu yoyote.

 Aliongeza kuwa baada ya muda kupita alikuja Muuguzi na kuwaeleza kuwa watoto wamefariki, kitu ambacho hakikuingia akilini mwake na kudai kuwa kuna uzembe umefanyika hadi watoto wake kupoteza maisha.

Baada ya kutokea sintofahamu ya kifo hicho usiku huo, walikubaliana waje kesho yake asubuhi kuchukua mwili kwenda kuzika na kudai walipofika asubuhi Muuguzi Paulo Makungu (37) aliwakabidhi miili hiyo na walipoifunua wakakuta mtoto 1 jicho limenyofolewa na ngozi ya uso imechunwa yote.

Alisema hali hii iliwasikitisha sana na kuzua taharuki kubwa ambapo walilazimika kwenda kutoa taarifa polisi na kufikisha habari hizo kwa Mkuu wa wilaya Dkt Rashid Chuachua, ambapo aliagiza kuchunguzwa kifo cha watoto hao.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Constantine Mbogambi amethibitisha kutokea tukio hilo na kubainisha kuwa miili ya vichanga hivyo 2 imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Urambo Mkoani hapa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa tukio lililoleta taharuki kubwa katika familia hiyo na wilaya nzima unaendelea na kubainisha kuwa wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha alipoulizwa kama kuna mtumishi au mtu yeyote anayeshikiliwa na Jeshi hilo kwa ajili ya mahojiano ya kuhusika na tukio hilo alisema bado hawajakamata mtu yeyote.