Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WATUMISHI 4 wa Kituo cha Afya Kaliua, wilayani Kaliua Mkoani hapa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha watoto mapacha waliofariki katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuzaliwa.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa njia ya simu jana Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian ameeleza kuwa uchunguzi wa kifo cha watoto hao waliozaliwa njiti Mei 9 mwaka huu majira ya saa 5 usiku katika kituo hicho umekamilika.
Alitaja watumishi wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo kuwa ni Asha Kajala (mhudumu aliyemzalisha mama usiku), Paul Makungu (mhudumu wa wodi), Benson Makaki (mhudumu aliyekabidhi miili asubuhi) na Therezia Kakiziba (mhudumu) .
Alisema awali walichukuliwa hatua watumishi 2 kwa kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi, lakini baada ya jalada la uchunguzi kukamilika watumishi wengine 2 waliokuwepo zamu usiku huo wameunganishwa katika kesi hiyo.
RC Batilda alisema jalada hilo limepelekwa kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali ili watuhumiwa wote 4 wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya na Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Rashid Chuachua na Jeshi la Polisi kwa kufuatilia ipasavyo suala hilo ikiwemo kufungua jalada la uchunguzi na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kifo cha watoto hao kimetokea katika wodi waliyokuwa wamelazwa licha ya kuzaliwa wakiwa wazima na kwamba hakuna ndugu yeyote wa watoto hao aliyewachukua wodini humo.
Aliongeza kuwa wazazi hawana na shaka juu ya kifo, kifo ni kazi ya Mungu, ila hawakubaliani na hali waliyoikuta kwenye miili ya watoto wao ambapo mmoja alikutwa amenyofolewa jicho1 na kuchunwa ngozi usoni, ulimi wenyewe upo.
‘Hii ndiyo dosari kubwa ambayo imeonekana na kuleta sintofahamu kwenye kifo cha watoto hao, tumemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwasimamisha watumishi hao wakati wakisubiri taratibu za kufikishwa mahakamani’, alisema.
Alitoa wito kwa wauguzi, watoa huduma za afya na watumishi wote kwa ujumla kuwa na hofu ya Mungu na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miiko ya taaluma yao ikiwemo kuwa na nidhamu na kutenda haki.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â