November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 7 nchini wanashida ya figo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha kuwa, asilimia 7 ya Watanzania wanaishi na ugonjwa wa figo nitoe na kutoa rai kwa wananchi kupima ugonjwa huo mara kwa mara ili kuepuka madhara yake makubwa ikiwemo gharama kubwa ya matibabu yake.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Mei 19, 2023 wakati akijibu swali la Mhe. Asia Abdukarimu Halamga katika Mkutano wa kumi na moja kikao cha 29, Bungeni Jijini Dodoma.

Ameendelea kusema kuwa, ugonjwa huu, kwa kiasi kikubwa unahusishwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari na maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Amesema, Katika kujali afya za Watanzania wakiwemo wenye ugonjwa wa figo, Serikali ya Rais Samia imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 290.9 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali za mikoa, katika vifaa hivyo vipo vifaa vya matibabu ya kusafisha damu (dialysis) kwa wagonjwa wa figo.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali ipo katika mpango wa kuona namna ya kupunguza gharama ya matibabu ya figo kupitia huduma ya kusafisha damu ili wananchi wenye uhitaji waweze kunufaika na huduma hizo, huku akiweka wazi kuendelea kuwatazama wasio na uwezo kabisa kupitia njia ya misamaha.

Sambamba na hilo Dkt. Mollel ameendelea kusisitiza kwa kuwataka Wabunge kuwa mabalozi wazuri wa kuiunga mkono Bima ya Afya kwa wote kwani ndio suluhisho la kudumu la matibabu ya magonjwa yote na huduma bora kwa kila Mtanzania kwa ngazi zote kuanzia zahanati mpaka hospitali ya Taifa.