Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WATOTO 3,870 wenye umri chini ya miaka mitano katika halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora wanatarajia kupatiwa chanjo ili kuwakinga na magonjwa yanayozuilika.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Zacharia Mwansasu alipokuwa akizindua zoezi la utoaji chanjo kwa watoto lililofanyika juzi katika Hospitali ya wilaya hiyo kwenye Maadhimisho ya wiki ya Chanjo.
Alisema chanjo ni muhimu sana kwa watoto wote walio na umri chini ya miaka 5 ili kuwalinda na magonjwa nyemelezi yakiwemo ya kuambukizwa, hivyo akawataka wazazi wote kuhakikisha wanapeleka watoto wote kuchanjwa.
Alifafanua kuwa chanjo hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali kukabiliana na magonjwa yanazuilika kwa chanjo kama vile Polio na Surua ikiwemo kuzuia vifo na ulemavu kwa watoto wote wenye umri huo.
Mwansasu alisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea na usambazaji wa chanjo na vifaa vya kutolea huduma hiyo na kuchukua sampuli za wahisiwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo surua, polio na rubella kwa ajili ya kuchunguza ili kudhibiti magonjwa hayo.
Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Wende Robert alitaja magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kuwa ni surua, polio, kifaduro, pepombunda, dondakoo, kuhara, homa ya ini na uti wa mgongo ambayo huathiri watu wa rika zote ila zaidi ni kwa watoto walio chini ya miaka 5.
Alisema njia kuu ya kuzuia magonjwa hayo hatarishi ni kupata chanjo dhidi ya magonjwa hayo kwa watoto waliochini ya miaka 5.
Aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawaleta watoto wao ili kupata kinga kamili ya afya zao dhidi ya magojwa hayo huku akisisitiza kuwa chanjo hiyo hutolewa bure mara nne au tatu kutengemea na aina ya chanjo.
 Wiki ya chanjo Duniani ilianza Aprili 25 mwaka huu imelenga kutoa chanjo za kawaida na za aina zote kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano zinazotolewa katika vituo vya huduma ya afya lengo ni kuhamasisha jamii kuwapeleka watoto kuchanjwa ili kukabiliana na magonjwa yanazuilika kwa chanjo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa