November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawataka VGS kutanguliza weledi katika shughuli za uhifadhi

Na Mwandishi wetu, timesmajira

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka Askari Wanyamapori wa Vijiji ( VGS) waliohitimu mafunzo ya kudhibiti matukio ya Wanyamapori wakali na waharibifu dhidi ya maisha na mali za wananchi katika maeneo yao kutumia mafunzo hayo waliyoyapata kwa maslahi mapana ya uhifadhi huku akisisitiza weledi na uaminifu wakati wakitekeleza majukumu yao

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha wakati akifunga mafunzo ya kozi kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji 120 katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii – Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma

Amewataka Askari hao wakawe chachu na suluhisho ya changamoto zinazowakabili wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu na wakatumie ujuzi walioupata katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za maliasili katika maeneo yao ili ziendelee kudumu kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo na si vinginevyo.

Aidha Dkt. Msuha amewahakikishia wahitimu hao kuwa, Wizara kupitia mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) imejipanga kuhakikisha kuwa wanawwezeshwa kwa namna yoyote ili waweze kutimiza majukumu ipasavyo katika maeneo yao.

Akizungumzia Mafunzo waliyopata askari hao, Mkuu wa Mafunzo ya Uhifadhi Maliasili Kwa Jamii, Bi Jane Nyau amesema ni pamoja na mbinu za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ambazo ni rahisi kuzitumia katika mazingira yao ya kawaida, hazitumii gharama kubwa kiuendeshaji na pia baadhi zinawapatia faida nyingine mbadala.

Naye Msimamizi wa Mradi wa REGROW, uliofadhili Mfunzo hayo, Dkt. Aenea Saanya amewashauri wahitimu hao Kutumia mafunzo waliyoyapata kwa kuanzisha vikundi vitakavyokuwa na miradi itakayoweza kuzalisha vifaa vinavyotumika katika kupambana na Wanyamapori wakali na Waaribifu kwenye maeneo yao kwani Mradi wa REGROW upo tayari kufadhili vikundi hivyo Kwa maslahi mapana ya uhifadhi nchini.

Askari hao 120 wa VGS waliohitimu Mafunzo ni kutoka Mikoa ya Dodoma (wilaya ya Chamwino), Pwani (wilaya za Rufiji na Kisarawe), Iringa (wilaya za Kilolo na Iringa vijijini) na Morogoro (wilaya za Kilombero, Mvomero, Kilosa na Morogoro vijijini)