October 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpogolo awataka viongozi wa CCM, Serikali ilala kushirikiana

Na Mwandishi Wetu.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam Edward Mpogolo, amewasisitizia viongozi wa kisiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa Serikali katika wilaya yake, kufanyakazi kwa kuzingatia mfumo wa kushirikiana kwa pamoja katika kujadili mipango ya maendeleo na changamoto za wananchi ili kufikia lengo linalokusudiwa na Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amewataka pia kusimamia kwa pamoja mipango na miradi ya maendeleo kwa karibu ili kuleta matokeo chanya kwa kuwa kutofanya hivyo kunasababisha mipango na miradi hiyo kukwama na hivyo wananchi kubaki wakimlaumu mtendaji mkuu wa Serikali ambaye ni Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

DC Mpogolo ameyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa CCM na wa Serikali kutoka Kata za Jimbo la Ukonga, akihitimisha ziara yake ya kujitambulisha kwao na kuwapa semina maalum ya kujenga uelewano wa kikazi kati yake na viongozi wa Chama na Serikali katika Wilaya yake.

Amesema, ulazima wa viongozi hao kushirikiana upo kwa sababu, viongozi wa CCM na Serikali wote wajibu wao wa kwanza ni kushughulikia shida au changamoto za wananchi.

DC Mpogolo, amesema, katika ushirikiano huo, kiongozi wa Serikali hapaswi kudhani kuwa shughuli zinazofanywa na kiongozi wa Chama kuhudumia wananchi hazimhusu au yule wa Chama kudhani shughuli zinazofanywa na kiongozi wa serikali hazimhusu.

“Nataka niwaambieni, uhusiano ulipo katika ya Serikali Kuu na hizi za chini na wananchi ni kwamba msingi wa uhusiano huu ni Wananchi, maana hakuna kiongozi ambaye anapatikana bila maamuzi ya mwananchi.

Tazama, ili Chama kishike dola, kinaingia katika Uchaguzi, katika uchaguzi huo watu ndiyo wanakipa ridhaa ya kukifanya kiunde Serikali, sasa Chama kikishaunda Serikali maana yake ni kwamba wewe kiongozi wa Serikali usingepatikana kama Wananchi wasingechangua Chama.

Kwa hiyo hapo maana yake ni kwamba hakuna kiongozi wa Serikali ambaye ataacha kujali shida za watu wakati ametokana na Chama ambacho kimepewa nafasi na watu, na hata kwa mujibu wa Katiba Wananchi ndiyo msingi wa Mamlaka”, amesema DC Mpogolo.