December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SMAUJATA : Wanawake tumieni mitandao ya kijamii kuongeza mtaji, wateja

Na Penina Malundo, Majira

SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA),imewataka wanawake wanapoelekea kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani kutumia matumizi sahihi ya Mitandao ya Kijamii katika kujielimisha na kuongeza wigo wa kukuza Mtaji na wateja kwa njia ya Mtandao ili kuweza kuongeza kipato chao.

Pia imewataka kutumia Teknolojia ya Mitandao kufuatilia habari katika vyanzo Sahihi vya Mambo ya Uchumi na Kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kushiriki fursa mbalimbali zinazopatikana katika Ofisi za maendeleo ya jamii na kuweza kuzitumia.Akizungumza hayo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa, Sospeter Bulugu , amesema kulingana na Kaulimbiu ya Mwaka huu ya siku hiyo “Ubunifu na Mabadiliko katika Teknolojia, iwe ni Chachu katika Kuleta Usawa wa Kijinsia” ,Shujaa wa Maendeleo inahamasisha Mwanamke kutenga muda wake kutafakari mchango wa teknolojia katika Shughuli zake za Kila siku hasa zile za kujiingizia kipato na kuongeza wigo wa uzalishaji mali.

Amesema wanawake wako nyuma kidigitali kuliko wanaume kwani takwimu zinaonesha katika nchi ambazo hazijaendelea,asilimia 76 ya watu wake japo wanafikiwa mtandao lakini asilimia 25 ndiyo wanakuwa online huku asilimia 52 kati ya hao wakiwa ni wanaume.

“Hii inaonyesha kuwa, kwa ulimwengu huu wa kidigitali wanawake wanaachwa nyuma katika masuala haya ya kidigitali na hakuna usawa wa kijinsia kwenye kutumia huduma za kidigitali,Sasa ni muda wa kuamka na kuanza kutumia fursa za kidigitali katika kuwaletea maendeleo,”amesema

Amesema kutokana na hali hiyo inaonyesha dhahiri kuwa wanawake wanaachwa nyuma katika masuala ya kidigitali.

”Inabidi kuwawezesha kielimu na Kiuchumi, ndiyo maana kwa nchi ya Tanzania Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katoa ada shuleni, anajenga Sekondari za wasichana mikoa yote kwa masomo ya sayansi na hii ni kufanya wanawake kuzidi kung’ara,”amesema na kuongeza

”Hadi sasa,Serikali inaendelea kutoa mikopo kwa wanawake ya asilimia 10 ya Mapato ya Halmashauri ambapo Wanawake wanatengewa asilimia 4 kati ya hizo fedha,na pia serikali imeweka mikakati tangu Mwaka 2000 kupitia sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ambapo imeeleza wazi mikakati itakayomwezesha mwanamke kujikomboa na hali duni kimaisha,”amesema.

Bulugu amesema katika ilani ya Chama Tawala cha Mapinduzi (CCM),imetaja masuala ya Usawa wa Kijinsia kama sehemu ya lengo la Serikali na pia zipo fursa nyingi tu kupitia taasisi za kifedha ambapo serikali imeelekeza Mwanamke kupewa kipaumbele katika nyanja zote.

“SMAUJATA inamshauri Mwanamke kuwa mwezi wa tatu utumike kwake kama mwezi wa kuweka malengo, jitihada na bidii katika kufikia ndoto ambayo anaiota kwa kuchagua kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, na matumizi sahihi ya mitandao,”amesema.

Kwa Upande wake Makamu Mwenyekiti wa Idara ya Habari na Mawasiliano SMAUJATA Taifa,Mwamini Samaje amesema kupitia siku hiyo wanawake waamke kuchangamkia fursa zinazopatikana katika ofisi za maendeleo ya jamii ili kuweza kufahamu ni mbinu gani wanaweza kutumia katika kujikwamua kiuchumi.

Amesema ili mwanamke aweze kuendelea na kuondokana na janga la unyanyasaji na ukatili lazima mwanamke aweze kujisimamia yeye mwenyewe bila kumtegemea mtu yoyote.

“Kwani chanzo cha ukatili ni umasikini ili uweze kujikwamua na umasikini huo,ni wajibu mwanamke kuchangamkia fursa zinazopatikana katika halmashauri mbalimbali nchini ambazo zinatoa mikopo nafuu,”amesema.

Amesema mikopo hiyo ni nafuu ambayo itaweza kumuwezesha mwanamke katika kujikwamua kiuchumi na hali ya sasa kuweka usawa wa kijinsia.

”Wanawake pia tunapaswa kuishi kwa upande na wenza wetu katika familia na kuondokana na usaliti kwani ndio chanzo kikuu cha watu kufanyiwa ukatili wa kuuliwa,kipigo na hata kuchomwa moto,”amesema.