October 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanginde: Wataalam wanaokwamisha miradi kutovumiliwa

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Chunya

UONGOZI wa Halmashauri ya Chunya umesema kuwa hautavumilia kuona miradi ya kimaendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya wataalam wachache ambao hawana lengo zuri la kuhakikisha miradi ya halmashauri inasonga mbele pamoja na ukosefu wa vifaa ikiwemo magari.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ,Bosco Mwanginde wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani la halmashauri hiyo liloketi kwa ajili ya kupitisha masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Mwanginde amewataka madiwani kwenda kusimamia makubaliano katika kuwatumikia wananchi ikiwemo ukusanyaji na usimamiaji mapato ya Halmashauri na kuagiza Ofisi za halmashauri kuhamia katika jengo jipya kufikia March 10, 2023.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya ,Mayeka Simon Mayeka ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kusimama kidete katika ukusanyaji mapato kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi kwenye miradi mbalimbali pamoja na Ushirikiano wanaompatia hata kuaminiwa na Mhe. Rais kuendelea kuongoza wilaya hiyo.

“Kuaminiwa na Rais Dkt.Samia najua ni kazi kubwa ninazofanya kwa kushirikiana na wakuu wa idara ambao ndo nguzo kuu katika ukusanyaji mapato ya Halmashauri ,naamini tutaendelea kuwa pamoja ndugu zangu tuendelee kushirikiana kwa pamoja katika kufanya kazi za wananchi “amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Chunya ,Noel Chiwanga amewapongeza madiwani na wataalam kwa kushikamana katika ukusanyaji wa mapato na kuwataka kuendelea kuwa waaminifu na waadilifu katika kufikia matarajio ya Serikali iliyoundwa na Chama hicho.

Pamoja na kushauri mambo mbalimbali ya kimaendeleo baadhi ya madiwani wameiomba Serikali kuendelea kutekeleza miradi mingineyo ipasavyo kwa maslahi ya wananchi wao.

Mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Chunya Bosco Mwanginde
Mkuu wa wilaya ya Chunya ,Mayeka Saimon Mayeka
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Chunya,Noel Chiwanga