Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Ili huduma katika sekta ya afya ziwe na tija kwa wananchi,wadau mbalimbali wanapaswa kuunga jitihada za serikali za kuhakikisha mahitaji na vifaa muhimu vinapatikana.
Hivyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya afya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Chama cha ushirika cha Nyanza Bottling Employee (NBE) kimetoa mashuka 50,yenye thamani ya 800,000, kwenye zahanati ya Nyakato.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mashuka hayo, Mwenyekiti wa chama hicho, David Otieno Okumu, ameeleza kuwa utoaji wa mashuka hayo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha vifaa kwenye huduma ya afya vinapatikana ili kuketa tija katika utoaji huduma bora ya matibabu.
Okumu ameeleza kuwa mbali na kuunga serikali mkono pia ni njia moja wapo ya kuzingatia sheria ya vyama vya ushirika ambayo inavitaka vyama vyote kutenga kiasi kidogo baada ya kupata faida kwaajili ya kuhudumia jamii.
“Kutoa msaada wa mashuka katika zahanati hii ni kuimarisha huduma zinazotolewa na serikali,pia tunapofanya shughuli za maendeleo tunapaswa kuhudumia jamii inayotuzunguka na sisi tunaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha jamii inapata huduma bora,”ameeleza Okumu.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa chama hicho kimekuwa kikitekeleza takwa hilo la kuhudumia jamii mara kwa mara ambapo kabla ya kuhudumia Zahanati ya Nyakato walishawahi kufanya hivyo pia katika kituo cha afya Igoma Wilaya ya Nyamagana.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga amekishukuru chama hicho na kuomba kisiishie tu katika zahanati hiyo badala yake kione namna ya kusaidia na maeneo mengine yenye uhitaji kwani uhitaji ni mkubwa huku akihimiza vyama vingine kuiga mfano huo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri yav Manispaa ya Ilemela ambae ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Charles Marwa, ameeleza kuwa serikali kupitia sera yake ya PPP inaruhusu wadau wengine kushirikiana nayo katika kuhudumia wananchi.
Hivyo chama hicho cha ushirika kisiishie katika kutoa mashuka badala yake kijikite pia katika kuchangia vifaa tiba na kuvifikia vituo vingine vya kutolea huduma za afya.
Ofisa Ushirika wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Theresia Chrisant,ameeleza kuwa NBE ni miongoni mwa vyama vikongwe vinavyopatikana ndani ya Wilaya ya Ilemela ambacho kina wanachama zaidi ya 450.
Ambacho kina mtaji wa zaidi ya bilioni 8 kilichoanzishwa mwaka 2001 hivyo kuviomba vyama vyengine kuiga mfano huo.
Mwakilishi wa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza Saguda Ngabi,aliahidi kuvilea na kuvisimamia vyema vyama vyote vya ushirika vilivyomo ndani ya Mkoa huo ili kuhakikisha vinatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotakiwa.
More Stories
Dkt.Mathayo:Dkt.Samia,Dkt.Mwinyi wanastahili,ajivunia mafanikio jimboni
Wanafunzi 3000 wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Rais Samia, Mwinyi ‘mitano tena’ Nchimbi aula