Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imebaini uchochoro wa mianya ya rushwa katika mfumo wa utoaji huduma kwa jamii na kuelekeza Mamlaka husika kuondoa mapungufu hayo mara moja.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Mussa Chaulo alisema wamebaini mianya hiyo baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa mifumo ya utoaji huduma ikiwemo warsha na utekezaji maazimio.
Alisema katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2022 jumla ya kazi 7 za uchambuzi wa mfumo zilifanyika ikiwemo warsha 5 na kufuatilia utekelezaji maazimio 5 ambapo walibaini mianya mingi ya upotevu wa mapato ya serikali.
Alisema mianya hiyo ipo kwenye mfumo wa uendeshaji masoko ya halmashauri ya manispaa Tabora ambapo ilibainika kasoro ya utozaji kodi tofauti kwa maduka yaliyopo eneo moja, uchakavu wa vibanda na ukosefu wa maegesho ya magari.
Kasoro nyingine ni kutokuwepo miundombinu mizuri ya kuondoa majitaka sokoni, kukosa utaratibu mzuri wa kusimamia usafi wa soko, halmashauri kutokuwa na ushirikiano na viongozi wa soko na halmashauri kutohusika na ulinzi wa soko.
Chaulo alitaja mianya mingine ya upotevu wa mapato kuwa ipo kwenye mfumo wa ukusanyaji tozo za madini ya ujenzi ambapo alibainisha kuwa hakuna ushirikiano mzuri baina ya Ofisi ya Madini na Ofisi ya Mkurugenzi wa manispaa.
Nyingine ni watoza ushuru kutokuwepo kwenye maeneo ya vizuizi vya magari na kwenye machimbo, wakusanya ushuru kuweka watu wao wasio na mashine za kielektroniki (POS) ambapo alipendekeza mawakala kutumika kukusanya mapato.
Aidha walibaini uwepo wa tozo kubwa kwa upande wa halmashauri ikilinganishwa na ile inayotozwa na Ofisi ya Madini ikiwemo wasafirishaji madini ya ujenzi kukwepa vituo vya ukaguzi na ukusanyaji mapato wakati wa usiku.
Ili kupunguza mianya hiyo inayopelekea kuwepo vitendo vya rushwa katika mifumo hiyo, tumeagiza Ofisi ya Mkurugenzi na Ofisi ya madini kuchukua hatua stahiki ikiwemo kufanyia marekebisho miundombinu iliyopo.
Aidha alibainisha kuwa wamefuatilia jumla ya miradi 25 ya maendeleo yenye thamani ya sh mil 30.6 katika sekta za afya, elimu na barabara, hakuna mapungufu yoyote waliyobaini.
Chaulo alisema wameendelea kutoa elimu ya rushwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili kupanua wigo wa uelewa, kufanya mikutano ya hadhara, kuendesha vipindi redioni, kuandika makala, kuimarisha klabu za wapinga rushwa, maonesho na semina pia wamenza utekelezaji programu ya TAKUKURU rafiki.
Aidha wamepokea jumla ya malalamiko 75 ambapo 57 yalikuwa na viashiria vya rushwa na 18 hayakuwa na viashiria na hatua zimechukuliwa, hivyo akatoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudhibiti vitendo hivyo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua