Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amepokea nakala za Hati za Utambulisho za mabalozi wateule wa nchi za Zambia, Brazil na Vatican.
Mhe. Waziri Tax amepokea nakala za Hati za Utambulisho za Balozi mteule wa Zambia nchini, Mhe. Mathew Jere, Balozi mteule wa Brazil nchini, Mhe. Gustavo Martins Nogueira na Balozi Mteule wa Vatican Nchini, Mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mabalozi hao kwa nyakati tofauti Waziri Tax amewahakikishia ushirikiano kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ya kibalozi hapa nchini. Pia Waziri Tax ametoa rai kwa mabalozi hao kuendeleza na kudumisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na nchi zao.
“Tanzania na Zambia tumekuwa marafiki na ndugu wa muda mrefu, Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zambia katika sekta za biashara na uwekezaji kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” alisema Dkt. Tax
Balozi mteule wa Zambia nchini, Mhe. Mathew Jere ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Zambia na Tanzania katika sekta za biashara na uwekezaji, usafirishaji, pamoja na nishati.
Kwa upande wake Balozi Mteule wa Brazil, Mhe. Gustavo Martins Nogueira ameahidi kuwa Brazil itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mapya ya kimkakati kwa manufaa ya mataifa yote mawili hususan kilimo, biashara na uwekezaji.
Naye Balozi wa Vatican nchini, mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino ameahidi kuendeleza kuimarisha ushirikiano mzuri uliopo baina ya Vatican na Tanzania.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato