Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET) kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri nchini (ATE), wamewapa tuzo kampuni na taasisi amabzo zimetoa mchango mkubwa kwenye uendelezaji ujuzi pahala pa kazi.
Tuzo hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiambatana na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda na Katibu Mtendaji wa NACTVET. Adolf Rutayuga
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hizo, Waziri Mkuu alisema kuna umuhimu wa kuwekeza kwa kiwango kikubwa kuendeleza rasilimali watu nchini ili taifa liweze kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kasi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa halfa ya kuwatunuku waajiri waliotoa mchango katika kuendeleza ujuzi kwa vijana wanaosoma kwenye vyuo vya ufundi.
Hafla hiyo iliandaliwa kwa pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET) ambapo waajiri mbalimbali walipewa tuzo.
“Mataifa yote duniani yaliyoendelea yamefanikiwa baada ya kuweka kipaumbele kwenye kuendeleza rasilimali watu kwasababu ujuzi unahitajika kwenye nyanja zote za uzalishaji mali na bila ujuzi hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana,” alisema
“Naipongeza NACTVET kwa kushirikiana na ATE kwa maandalizi mazuri ya hafla hii ya kuwatuza waliotoa mchango kwenye uendelezaji wa ujuzi naamini mafanikio ya shughuli hii ni matokeo ya mshikamano baina ya sekta binafsi na umma,” alisema
Aidha, aliwapongeza waajiri na wadau wote walioshirikiana na NACTVET kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata ujuzi stahiki unaotakiwa kwenye soko la ajira la ndani na la kimataifa.
“Nimefurahi kusikia jitihada za serikali kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya kujiajiri mmeiwekea mipango ya kuitekeleza kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kujiajiri wanapomaliza mafunzo yao,” alisema
Aliwapongeza waajiri nchini kwa nafasi wanayotoa kwa wanafunzi kufanya kazi kwa vitendo kwani wenyewe wamekiri kwamba wananufaika na mafunzo hayo kwani yanawaongezea ujuzi mkubwa.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri (ATE) Suzzane Ndomba, alisema chama cha waajiri kimeendelea kuunga mkono juhudi mbali mbali za Serikali kwenye kukuza ujuzi na kuchochea ukuaji wa ajira hapa nchini katika mipango yetu.
Sambamba na kuhamasisha waajiri kushiriki katika programu ya kitaifa ya uanagenzi inayoratibiwa na TAESA.
Alisema wameendelea kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo ikiwemo GIZ Tanzania na Shirikisho la Waajiri kutoka nchini Denmark (Confederation of Danish Industries) kutekeleza miradi ya ujuzi hapa nchini na hasa katika mikoa ya Lindi, Manyara, Dodoma, Morogoro na Dar-es-Salaam, yenye lengo la kuwapatia ujuzi vijana ili waajirike.
“Kupitia mradi wetu na GIZ vijana 4500 kutoka Lindi, Manyara and Dodoma watapatiwa mafunzo katika ufundi bomba (viwandani na majumbani), uchomeaji (viwandani na majumbani) na mechatronics. na kati ya hao wahitimu 1800 wataunganishwa na makampuni kwa ajili ya mafunzo. Hii itakwenda sambamba na uhuishaji wa mikataba 50 baina ya waajiri na VETA ili waweze kundeleza mashirikiano hata baada ya mradi,” alisema.
Alisema bado tunaamini, ili Tanzania iweze kushiriki kikamilifu katika soko shindani la Afrika Mashariki na dunia nzima, ni lazima kuchukua hatua za maksudi katika kukuza ujuzi hususani kwa vijana.
Alisema katika kutimiza adhma hiyo ATE inaaamini waajiri wana nafasi kubwa katika kufikia malengo waliyojiwekea kama nchi mfano kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, awamu ya tatu (“the National Five-Year Development Plan-Phase three), tumelenga kupunguza ukosefu wa ajira kutoka asilimia 9 (mwaka 2019) kufikia asilimia 8 ifikapo mwaka 2025/26.
“ Kukuza ujuzi ni kati ya mipango iliyobainishwa na Serikali ili tufikie lengo na kuongeza idadi ya wahitimu waliopata mafunzo mahala pa kazi ni njia mojawapo ya kukuza ujuzi nchini kwa vijana wetu. Kwa mfano, kama nchi tunatazamia kuongeza idadi ya wahitimu wenye mafunzo ya uanagenzi kufikia 231,000 ifikapo mwaka 2025/26 kutoka 46,000, mwaka 2019/20. Vivyo hivyo, kwa mafunzo tarajari, lengo ni kufikia wahitimu 150,000 ifikapo mwaka 2025/26 kutoka 30,000, mwaka 2019/20,” alisema.
“Mwaka jana, katika hafla kama hii, ATE tuliwasilisha ombi la kuwapa unafuu waajiri ili waweze kushiriki kikamilifu katika adhma hii ya kukuza ujuzi nchini na tuliomba Serikali itoe unafuu katika malipo ya tozo ya ujuzi (SDL) kwa waajiri ambao watapokea wahitimu kutoka vyuo vikuu na vyuo vya ufundi kwa ajili ya mafunzo ya tarajali (internship) kupitia Taasisi ya TAESA” alisema.
“ Kwenye hili tuliomba gharama au malipo yoyote yanayotolewa na waajiri kwa wanufaika wa program hii, kwa mfano posho za kujikimu yasiwe sehemu ya kukokotoa malipo ya SDL. Kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 (the Finance Act 2022), pendekezo hili lilifanyiwa kazi. Naomba nitumie, fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuliona hilo na kulifanyia maboresho,” alisema.
Alipongeza unafuu waajiri waliopata kwa punguzo la tozo ya WCF kutoka asilimia 1 mpaka asilimia 0.5. kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 na kwamba suala hili limeleta usawa katika uchangiaji wa tozo hii kati ya Sekta ya Umma na Binafsi.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti