December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA kujenga Km 2 za barabara ya lami Kaliua

Na Allan Vicent, TimesMajira Onlie, Kaliua

WAKALA wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilayani Kaliua Mkoani Tabora anatarajia kujenga barabara ya lami yenye urefu wa km 2.2 katika Mitaa mbalimbali wilayani humo ili kuboresha zaidi mandhari ya Mji huo.

Akizungumza na gazeti hili juzi Meneja wa Wakala huo Wilayani hapa Mhandisi Kisandu Robert alisema mradi huo utatekelezwa katika mwaka ujao wa fedha kwa gharama ya sh bil 1.5 zikiwa ni fedha za tozo ya mafuta.

Alitaja barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni Market-Mawese yenye urefu wa km 0.33, Machinjio yenye urefu wa km 0.27, AICMji mwema (km 0.38), Inakwetu (km 0.18) na barabara ya Chuo yenye urefu wa km 0.44.

Mbali na mradi huo alisema wanatarajia kuwa na miradi mingine ya matengenezo maalumu na ya kawaida kwa barabara korofi zote ili kuziwezesha kupitika wakati wote, matengenezo hayo yatahusisha ujenzi wa makalvati na mitaro.

Alibainisha barabara zitakazofanyiwa matengenezo ya kawaida na kujengewa makalvati na mitaro kuwa zitakuwa na urefu wa km 53.3 na zimetengewa jumla ya sh mil 928.56 za mfuko wa barabara.

Aliongeza kuwa barabara zitakazotengenezwa kwa kiwango cha changarawe ikiwemo kujengewa mitaro na makalvati zina urefu wa km 36 na zitagharimu kiasi cha sh bil 1 za mfuko wa jimbo, barabara hizo zipo katika kata za Usinge, Sasu, Mwongozo na Seleli.

Barabara nyingine zitakazojengwa kwa kiwango cha changarawe zenye urefu wa km 53 zipo katika kata ya Uyowa, Kashishi na Ulyankulu na zimetengewa sh bil 1.5 za tozo ya mafuta.

Mhandisi Kisandu alifafanua kuwa katika mwaka ujao wa fedha wanatarajia kutumia kiasi cha sh bil 4.9 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zote katika wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara za lami.