Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Wilaya ya Ilemela imetakiwa kuhakikisha inakamilisha miradi yote ya kupunguza umaskini(TASAF) sanjari na kuanza kufanya mikutano katika mitaa kwa ajili ya tathmini ya walengwa wa mpango huo.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Jenista Mhagama, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, Februari 29,2023 kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF III katika Wilaya ya Ilemela, ambapo amekagua mradi wa ujenzi wa zahanati ya Mihama pamoja na nyumba ya mtumishi.
Ambapo ameeleza kuwa wana kila sababu ya kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika mapema na kuanza kutoa huduma kwa wananchi
“Lazima tutarudi hapa,Aprili mwaka huu ili kuona zahanati hii inaanza kazi hatuna sababu ya kuchelewesha miradi hii mikubwa kama hii inayojibu kero na mahitaji makubwa ya wananchi wetu hususani wanawake, watoto na wazee,”ameeleza Mhagama.
Ameeleza kuwa miradi hiyo 10, itakapo kamilika wataleta miradi mingine kumi kupitia fedha hizo za OPEC chini ya TASAF,hivyo wahakikishe miradi hiyo inakamilika mapema.
“Mifumo imefunguka, fedha zipo na wananchi wapo, hivyo kamilisheni miradi hii kwa haraka, ameeleza Mhagama.
Sanjari na hayo ametumia fursa hiyo kufafanua juu ya malalamiko ya walengwa wa TASAF wasiokuwa na sifa ambapo ameeleza kuwa amewaeleza jambo hilo la mtu ambae hana sifa lipo mikononi mwao wananchi na utaratibu wa kumchagua mwenye sifa unafanyika kwenye mitaa yao.
Hivyo akatoa maagizo kwa uongozi wa Ilemela kuanza kufanya mikutano katika mitaa kwa ajili ya kufanya tathmini ya walengwa wa TASAF.
“Mkuu wa Wilaya simamia suala hili, fedha hizi anatakiwa apate mlengwa ambae anazingatia vigezo,kila mtu akimuona aone kuwa anastahili kutunzwa na mfuko wa TASAF,”.
Aidha ameeleza kuwa,mfuko wa TASAF ni mzuri ambao lengo lake ni kuhakikisha kila Mtanzania anaweza kushiriki katika ujenzi wa uchumi wake binafsi na taifa kwa ujumla.
“Pamoja na TASAF kuwa inatoa ruzuku, Mkurugenzi nikuelekeze uvitambue vikundi kwa walengwa hawa wa mfuko huu,na wenyewe wapewe mikopo ya asilimia kumi ya Halmashauri isiyo kuwa na riba,”ameeleza Mhagama.
Mratibu wa TASAF Wilaya ya IlemelaLeonard Robert, ameeleza kuwa mradi huo utakapo kamilika unatarajia kugharimi kiasi cha milioni 219.25, ambao utasaidia kusogeza huduma ya afya ya uzazi, maendeleo ya mtoto na lishe karibu zaidi na wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima, ameeleza kuwa hadi kufikia Machi,28,2023 watakuwa wanekamilisha miradi hiyo ili wananchi waanze kupata huduma ya afya ya mama na mtoto pamoja na lishe.
Diwani wa Kata ya Kitangiri Donald Protas, ameeleza kuwa TASAF imeweka historia kwenye kata yao,imechangia Kata hiyo kuanza kuwa na maendeleo kwa kasi katika sekta ya afya , huku akiwapongeza wananchi kwa namna ambavyo wamejitolea kuhakikisha zahanati hiyo inajengwa .
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala, amemshukuru Rais kwa kuwaletea miradi ya TASAF wananchi wa Kata ya Kitangiri ambayo imekuwa chachu kwenye maendeleo.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia