Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
JESHI la Polisi Mkoani Tabora limekamata watu 3 na kuwapandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Tabora kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara wa mazao ya nyuki.
Waliopandishwa kizimbani juzi na kusomewa shitaka hilo ni Feruz Abdalah Feruzi, Masumbuko Said Ramadhan na Tumba Shabani.
Upande wa Mashitaka ukiongozwa na Wakili Joseph Mwambwalulu ulidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo Julai 14/2022.
Aliongeza kuwa siku hiyo majira ya saa 4 asubuhi eneo la Kazuge, Kata ya Mpera watuhumiwa walimuua kwa kumpiga risasi Mohamed Mustapha Ngendela akiwa nyumbani kwake.
Aliongeza kuwa siku hiyo mara baada ya kutenda kosa hilo watuhumiwa walifanikiwa kutoroka lakini jeshi la polisi liliendelea na msako na kufanikiwa kuwakamata na kuwafungulia shitaka linalowakabili.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hivyo likaahirishwa hadi Februari 14 itakapotajwa tena, watuhumiwa wote wamepelekwa rumande hadi siku hiyo.
Ilielezwa kuwa siku ya Tukio watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walifika nyumbani kwa Mohamed Mustapha Ngedela ambaye kwa sasa ni marehemu na kumpiga risasi akiwa nje ya nyumba yake na kutoweka kwa kutumia usafiri wa bodaboda.
Tukio hilo liliwaacha midomo wazi majirani kwani wauaji hawakuchukua kitu chochote nyumbani kwa mfanyabiaashara huyo na kuamua kutokomea kusikojulikana hadi walipokamatwa na polisi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba