September 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau watoa tamko, mtoto kutumikishwa kazi za nyumbani

Na Judith Ferdinand, Timesmajira online Mwanza

Shirika la WoteSawa kwa kushirikiana na wadau wanaotetea haki za binadamu nchini Tanzania,wametoa tamko la kulaani kitendo cha kikatili kinachodaiwa kufanywa na Mwalimu cha kumuajiri mtoto chini ya umri unaoruhusiwa kisheria.

Taarifa ya tamko hilo ambao imetolewa Februari 3,2023 na Shirika la WoteSawa pamoja na wadau wengine,imeeeleza kuwa wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kitendo cha utumikishwaji wa kazi za nyumbani kwa mtoto mwenye umri wa miaka 10 kinachodaiwa kufanywa na Mwalimu Diana Mwaihoji wa Shule ya Msingi Ilendeje ya` Kisesa Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.

Ambapo tamko hilo limeeleza kuwa mnamo Februari Mosi mwaka huu, mitandao mbalimbali ya kijamii iliripoti video iliyoambatana na taarifa ya binti huyo aliyedaiwa kutoroka na mtoto mdogo wa mwajiri wake kuelekea nyumbani kwao jijini Mbeya.

Taarifa hiyo ilidai mtoto huyo aliokolewa katika kituo cha mabasi cha Nyegezi jijini Mwaza hivyo baada ya kupokea taarifa hiyo,shirika la WoteSawa lilifanya ufuatiliaji wa tukio hilo kwenye mamlaka husika za Polisi na Idara ya Ustawi wa Jamii na kubaini kwamba, mtoto huyo yuko chini ya uangalizi wa ustawi wa jamii na mwajiri wake akiwa ameshikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.

Kwa mujibu wa tamko hilo imeeleza kuwa , Februari,3 mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilitoa taarifa kupitia Kamanda wake Wilbroad Mutafungwa kwamba, mtoto huyo alisafirishwa na mwajiri wake kutoka kwa wazazi wake mkoani Mbeya kwa lengo la kumsaidia kazi za nyumbani kwa ahadi ya kumuendeleza kimasomo,jambo ambalo halikufanyika.

Pia taarifa hiyo ilidai kuwa, mtoto huyo alikuwa akifanyiwa vitendo vya kikatili vya kuchapwa mara kwa mara, hali iliyopelekea binti huyo kutoroka.

“Tunaipongeza serikali kupitia Jeshi la Polisi na Idara ya Ustawi wa Jamii kwa hatua zilizochukuliwa ikiwemo kumkamata mtuhumiwa, kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kumpatia mtoto huyo hifadhi ya muda wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea,”imeeleza sehemu ya tamko hilo.

Pia tamko hilo limeeleza kuwa pamoja na hayo, kitendo cha kumtoa mtoto huyo kwa mzazi wake alikokuwa anasoma kwa ahadi ya kumuendeleza kielimu na badala yake kumuajiri akiwa na umri wa miaka 10 ni kinyume cha sheria na kimemnyima haki zake za msingi ikiwa ni pamoja na haki ya kupata elimu.

Huku kitendo cha kumfanyia ukatili wa kimwili wa kumchapa mara kwa mara, kimesababisha madhara ya kimwili na kisaikolojia kwa mtoto huyo.

Aidha , kitendo cha kurekodi na kusambaza taarifa hiyo kimetweza utu wake, kimezua taharuki, kuleta mtazamo hasi dhidi ya mtoto huyo na kinaweza kumletea athari katika makuzi na maendeleo yake.Sanjari na hayo taarifa hiyo imeeleza kuwa licha ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali pamoja na wadau ikijumuisha uwepo wa dheria na sera zinazomlinda mtoto, kusimamia ajira kwa wafanyakazi wa nyumbani na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Bado kumekuwa na changamoto kubwa ya watoto kuajiriwa katika umri mdogo, kutokulipwa mishahara stahiki na kwa wakati, kutendewa ukatili na unyanyasaji pamoja na wimbi la watoto kuwa wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Hata hivyo taarifa hiyo imetoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo Serikali kupitia mamlaka husika itekeleze kikamilifu Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 sambamba na Mkataba wa Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) Na.138/1973; unaoweka katazo la ajira kwa watoto chini ya miaka 14.

Serikali kupitia mamlaka husika kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya watu wanaoajiri watoto chini ya umri uliowekwa kisheria, kuajiri bila kuwa na mkataba wa maandishi, kulipa mshahara chini ya kiwango au kutokulipa kabisa.Serikali iridhie Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Nyumbani namba 189/2011 na kuweka sheria maalum itakayosimamia ajira ya kazi za nyumbani.

Vile vile mamlaka husika za serikali zisimamie kikamilifu sheria na mifumo ya kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, hususani kwa watoto huku waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani wazingatie sheria za ajira ili kuwezesha uwepo wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani.

Huku wazazi wazingatie wajibu wao katika malezi ili kulinda haki na maslahi ya watoto, hususani haki ya kupata elimu pamoja na wananchi waache vitendo vya kurekodi na kusambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii, badala yake watoe taarifa kwenye mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe na waendelee kupaza sauti na kuripoti vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto na wafanyakazi wa nyumbani.

Tamko hilo limetolewa na wadau wa haki za binadamu ambao ni shirika la WoteSawa Domestic Workers Organization,Railway Children Africa,The Light for Domestic Workers, Initiative for Domestic Workers, New Hope, New Winners Foundation,Tanzania Child Domestic Workers Coalition,Coalition for Women Human Rights Defenders – Tanzania,Tanzania Coalition Against Child Labour na Haki Sawa Domestic Workers Organization.