Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
KAMATI ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto (MMMAM) mkoani Dodoma imekutana kwa ajili ya kikao cha tathimini ya robo ya pili ya mwaka katika utekelezaji wa Mtoto Kwanza unaoangazia suala zima la Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambapo imebaini moja ya changamoto ya utelelezaji wa masuala ya MMMAM ni ukosefu wa fedha.
Aidha kikao hicho kimezungumzia kuhusu uwepo wa vitabu shuleni vyenye mafundisho yaliyo kinyume na maadili hali ambayo inachangia kudhorotesha hali ya malezi,makuzi na maendeleo ya watoto.
Kufuatia hali hiyo kikao hicho kimeazimia kwenda kuhamasisha ili bajeti ya utekelezaji wa MMMAM iweze kuingia kwenye mipango ya halmashauri hizo lakini pia kuendelea kuhimiza wadau wa masuala ya Malezi na makuzi ya watoto kuendelea kuhamasisha jamii umuhimu wa kuwa karibu na watoto wao ili kujua maendeleo ya ukuaji wao.
Akizungumza jijini Dodoma, Afisa Maendeleo ya Vijana Mkuu,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Tumaini Mwasamale aliyeongoza kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa hu Dkt.Fatma Mganga alisema,ukosefu wa fedha umeonekana ni moja ya changamoto inayokwamisha utekelezaji wa masuala ya MMMAM .
“Zipo changamoto kadhaa kwenye utekelezaji wa mpango hususan za kibajeti na upatikanaji wa taarifa,hata hivyo katika kikao hiki tumezipitia na kuweka mkakati wa pamoja wa kuzitatua ikiwa ni pamoja na halmashauri kuupa umuhimu mpango huo kwa kuuingiza kwenye bajeti zao ili kuwezesha utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ambayo inatekelezwa nchini kote.”amesema Mwasamale
Vile vile amesema pia kikao hicho kimeazimia kuimarisha uhusiano na wadau wanaotekeleza mpango huu ,ili wafanye kazi kwa karibu na kuwezesha upatikanaji wa taarifa pamoja na na kuendelea kushirikisha wadau wengi zaidi wakiwemo wakiwemo viongozi wa dini ili kupanua wigo wa kufikisha ujumbe wa MMMAM kwa jamii.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na watoto Polisi mkoa wa Dodoma Yasinta Kayombo amesema,bado kuna changamoto kwenye malezi na makuzi ya watoto inayosababishwa na utandawazi kupitia simu za mkononi na Televisheni.
Ametumia nafasi hiyo kuwaasa wazazi kukagua na kufautilia katuni,tamthilia pamoja na nyimbo wanazoangalia watoto kwenye televisheni au kwenye simu za kiganjani kwani vimekuwa ni moja ya vitu vinavyochangia katika kuharibu na kurudisha nyuma jitihada za malezi na makuzi ya watoto zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau.
“Wakati Serikali inapambana kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka 0-8 ,lakini bado kuna changamoto hasa zinazotokana na utandawazi,watoto wamekuwa wakitumia simu za kiganjani za wazazi wao au Televisheni kuangalia katuni ,tamthilia na hadithi mbalimbali,
“Lakini mwisho wa siku katikati ya katuni hizo au tamthilia na nyimbo kumekuwa na maneno ama vitendo ambavyo havina maadili ambavyo watoto hawa ambao ni wadogo wanajifunza na kushika haraka sana na hivyo kuchochea vitendo vya ukatili baina ya watoto kwa watoto na hivyo kuathiri Malezi na makuzi yao kwa namna moja ama nyingine.”amesema Kayombo
Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknlojia akizungumza jijini Dodoma kupitia Katibu Mkuu wake Dkt.Francis Michael anaelezea kuhusu uwepo wa vitabu hivyo huku akiwataka wamiliki wote wa shule hapa nchini kuzingatia waraka namba nne ambao unatoa muongozo katika shule zote nchini kuzingatia ubora wa elimu inayotolewa vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa wahuska ikiwemo kufungia usajili wa shule husika.
“Wizara katika kutekeleza wajibu wake kwa kusimamia utoaji wa elimu nchini na katika kuhakikisha kuwa njia mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji zinazingatia ubora,maslahi ya nchi,mila ,desturi na tamaduni za watanzania ilitoa waraka namba nne wa mwaka 2014 ambao pamoja na sheria na nyaraka nyingine na miongozo inayohusu elimu ulilenga katika kuhakikisha kuwa vitabu bora vya ziada na kiada vinavyotumika katika shule zote zilizosajiliwa nchini na siyo vinginevyo,
“Vitabu vinavyotumika katika ngazi zote za elimu kuanzisa shule za msingi ni vyenye maudhui yanayoendana na mila ,desturi na utamaduni wa nchi yetu na kuweza kumlinda mtoto wa kitanzania aliyepo shuleni.”amesema na kuongeza kuwa
“Katika kusimamia utekelezaji wa waraka huu,wizara imebaini kuwa kuna baadhi ya shule ambazo zimekuwa zikiingiza na kutumia vitabu ambavyo maudhui yake yanakinzana na mila,desturi ,miongozo pamoja na tamaduni za kitanzania ambapo maudhui hayo yanahatarisha ukuaji na malezi ya watoto na pia kupotosha mila na desturi za nchi yetu.”
Naye Afisa Maendeleo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Chemba Madlina Kalinganira alisema,kwa upande wao wanaendelea kutekeleza PJT-MMMAM kwa kushirikiana na wadau hususan wanaotekeleza afua za watoto wilayani humo kwa lengo la kufikisha elimu ya MMMAM kwa jamii.
Vile vile amesema,pia wanaendelea kushirikiana na viongozi wa dini na kwa kushirikiana na divisheni nyingine kama afya,lishe,elimu,ustawi wa jamii ,pia kuweka katika mipango ya halmashauri kwa kuingiza kwenye bajeti ili iwe rahisi kwa ajili ya utekelezaji.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Oliver Njogopa,amewaasa wadau hao kuendelea kufuatilia na watoto wenye ulemavu kwani nao ni miongoni mwa watoto wanaopaswa kulelewa kwa kuzingatia afua tano za Afya,lishe,ujifunzaji wa awali,ulinzi na usalama wa mtoto pamoja na Malezi yenye mwitikio.
Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) 2021/22-2025/26 ,inatakiwa izingatiwe na afua zote za malezi zitekelezwe kwa ujumuishi kwa kuwa programu hiyo inalenga kuleta matokeo chanya katika ukuaji na maendeleo ya awali ya mtoto na kufikia maono.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM