November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yaridhishwa na maendeleo ya mradi wa maji Butimba

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Kilimo,Mifugo na Maji,imewataka watu wote wanahusika katika kufanya kazi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba watimize wajibu wao ili mradi huo ukamilike.

Huku ikiridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo uliopo wilayani Nyamagana mkoani hapa ambao ukikamilika utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa maji kwa wakazi wa Jiji la Mwanza.

Ambacho ndicho kimekuwa kilio chao cha muda mrefu kinacho sababishwa na ongezeko la watu kuwa kubwa kuliko uwezo wa miundombinu ya uzalishaji maji kwa siku iliopo sasa yenye kuzalisha lita milioni 90 huku uhitaji ukiwa lita za maji milioni 160.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 za maji kwa siku, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Almas Maige, ameeleza kuwa maendeleo ya mradi ni mazuri kazi imefanyika na fedha imetumika kama zinavyotakiwa.

Ameeleza kuwa mradi huo ambao wanaimani utakamilika na kutoa lita za maji milioni 48 na kujaziliza upungufu wa maji kwa Jiji la Mwanza hivyo utakuwa tiba kwa wananchi kupata maji.

Huku akieleza kuwa kwa mujibu wa wataalamu utaongezeka na kuzalisha lita za maji milioni 160 ili kukidhi mahitaji ya maji kwa mji huo ambao unaongezeka lakini hakuna mbadala wa maji.

“Mimi na Kamati yangu tumeridhika kwamba hapa kazi inafanyika na fedha zinatumika kama vile ambavyo zimekusudiwa,nataka kusema wote wanaofanya kazi hapa watimize wajibu wao kwani kilio cha Rais Samia ni kumtua mama ndoo kichwani na mimi naongezea na mitungi kichwani,”ameeleza Maige.

Aidha ameeleza kuwa Wakandarasi wanaochelewesha miradi hawana nafasi ya kufanya kazi nchini hapa kwani kuna sheria nzuri inayowabana wakandarasi wanaochelewesha miradi.

“Lakini hapa mradi kama umechelewa zipo sababu ambazo siyo za wakandarasi nasi tumefuatilia na tunajua jambo linalotokea ambalo halihusu pande mbili ambazo zimekubaliana kwenye mkataba mradi huu unaenda vizuri,”ameeleza Maige.

Naibu Waziri wa Maji MaryPrisca Mahundi ameeleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa Mkoa wa Mwanza hivyo Wizara imepokea maagizo yote yaliotolewa na Kamati hiyo.

Hivyo watausimamia mradi huo kwa ukaribu zaidi tofauti na awali ili kuhakikisha unakamilika mapema lengo lao ni kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa uharaka.

“Kamati hii imekuwa ikitishauri na kufanikiwa sana na hapa Mwanza kwenye huu mradi ni mradi ambao tunautegemea uongeze tija katika kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo haya na tunaendelea kufuatilia kuhakikisha vifaa vinafika ndani ya muda ambao tumekubaliana na hatuwi kikwazo kuona mradi huu unakamilika,”ameeleza Mahundi.

Akitoa taarifa ya Mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele, ameeleza kuwa mradi mzima una njia (line) 4 zenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 160 kwa siku.Lakini awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo wameanza na njia(line).

Moja ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku na umegharimu kiasi cha bilioni 69 na kunufaisha wananchi takribani 500,000.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mjumbe wa kamati hiyo Emmanuel Cherehani, ameeleza kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa Mwanza na ukanda wa Ziwa Victoria hivyo Wizara ya Maji inapaswa kuzingatia ipasavyo mikataba iliyowekwa.”

Mkandarasi asimamiwe fedha za umma ambazo Rais amezitoa ziweze kuwanufaisha wananchi kwa wakati kwa sababu wanauhitaji mkubwa wa huduma ya maji,” ameeleza Cherehani.

Huku akiishauri serikali kuwaangalia na kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani waweze kupewa mikataba ya kandarasi ya miradi mikubwa ya maji,barabara na mingine ili kuendelea kuwajengea uwezo mkubwa badala ya kuendelea kuwapa nafasi wakandarasi kutoka nje ya nchi pekee.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza unaupungufu wa maji lita million 70 japokuwa wanamiradi ya maji yenye thamani ya billioni 300 ikiwemo iliyokamilika pamoja na inayoendelea na utekelezaji malengo yao ni kuhakikisha wanamaliza tatizo la maji.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza(MWAUWASA) Mhandisi Leonard Msenyele akitoa maelekezo kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji iliiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Almas Maige, walipotembelea mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba kilichopo jijini Mwanza.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na na Almas Maige, wa pili kushoto akiwa na Naibu Waziri wa Maji MaryPrisca Mahundi wa pili kulia na wajumbe wengine wakati Kamati hiyo ilipotembelea mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba kilichopo jijini Mwanza.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza(MWAUWASA) Mhandisi Leonard Msenyele akitoa maelekezo kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji iliiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Almas Maige, walipotembelea mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba kilichopo jijini Mwanza.
Muonekano wa baadhi ya maeneo mbalimbali ya mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba unavyoonekana.